
BOSI wa lebo ya muziki ya WCB Wasafi, Diamond Platnumz amefunguka kwa mapana na marefu sababu itakayomfanya kutomlipisha msanii wake Mbosso pindi atakapotaka kuondoka katika lebo hiyo.
Kauli yake inajiri kipindi ambapo kumezagaa tetesi kwamba Mbosso yuko mbioni kuondoka WCB Wasafi na kuwa msanii huru.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano jijini Dodoma wakati wa mkutano wa kisiasa wa chama tawala CCM nchini Tanzania, Diamond alifichua kwamba ni kweli wamekuwa na mazungumzo na Mbosso kuhusu yeye kutaka kuondoka WCB.
Alisema kwamba ikiwa Mbosso atafikia uamuzi wa kuondoka, basi yeye hatoshrutishwa kulipa kiasi kisichokuwa chini ya milioni 500 – ambacho kimekuwa kama utaratibu wa WCB Wasafi kwa msanii yeyote anayetaka kugura.
“Wiki mbili zilizopita nadhani tumeongea na Mbosso na aliniomba aanze kujisimamia na nikampa Baraka zote. Mbosso ni mdogo wangu. Kwanza sababu ya mimi kumsaini Mbosso ilikuwa mimi nampenda sana. Mimi na yeye hatujawahi gombana,” Diamond alisema.
Kando na upendo wa ‘kikaka’ baina yake na Mbosso, Diamond pia alisema sababu nyingine ni kwamba msanii huyo tangu kuingia Wasafi hawajawahi kwanzana na amekuwa akimuonyesha heshima kubwa sana.
“Nilimwambia ‘mdogo wangu kwa jinsi ulivyoniheshimu, kwa ulivyonipenda na tulivyopendana siwezi kukutoza hata shilingi 10’. Kwa hiyo sijamtoza hata shilingi 10 na nafikiri mpaka sasa hivi tumeshakamilisha vitu vyote tayari ameshaanza kujisimamia rasmi,” Diamond aliongeza.
Licha ya kumalizana na WCB Wasafi, Diamond alikinai kwamba Mbosso bado atasalia kuwa mmoja wa wanafamilia wa Wasafi na hatoacha kumpigania kimuziki kisa hayuko Wasafi tena.
“Lazima tumuunge mkono, lazima tumsapoti na ataendelea kuwa familia ya Wasafi na nitaendelea kuhakikisha kwamba nampigania na kumlinda sehemu naweza kumlinda.”
Diamond alisema kwamba Mbosso ni mmoja kati ya wasanii wachache ambao wameweza kutumia hekima katika kutafuta mwafaka wa kuondoka na kumpa hongera yake.
“Unajua ni wasanii wachache sana wanaweza kutumia hekima kama yeye. Alipokuja Mbosso alikuja akiwa tayari kulipa ili kuruhusiwa kuondoka. Nilimwambia ‘mdogo wangu mimi siwezi kukutoza’. Kwa heshima na mapenzi aliyonionyesha kumtoza hela Mbosso kwangu mimi itakuwa ni aibu. Lakini angekuwa mtu mwingine ama hatujaheshimiana, aah hela unatoa!” alihitimisha.