
RAIS William Ruto amevunja kimya chake baada ya wakenya kugeuza hotuba yake ya kuzindua barabara ya kilomita 750 kaskazini mashariki mwa Kenya kuwa wimbo wa kejeli.
Wakenya wa matabaka mbalimbali kwenye mitandao wa TikTok
waligeuza hotuba ya Ruto kutaja Maeneo ambayo barabara ya kilomita 750 itapitia
kuwa wimbo kama njia moja ya kukejeli ahadi hiyo.
“Ndio barabara itoke
Mandera, ikuje Rhamu, ikuje Garre, iende Elwak, ikuje Kobow, ikuje Kotulo, ikuje
Tarbaj, ipitie pale Wajir, iende Samatar, iteremke Modogashe, ifike Isiolo,” Ruto alisema wiki tatu
zilizopita wakati wa ziara ya wiki moja ya kimaendeleo katika ukanda wa Kaskazini
mashariki.
Ni kauli ambayo iliwavutia Wakenya wengi haswa kwa jinsi rais
alikuwa na ustadi katika kujua Maeneo mbalimbali ya eneo hilo ambalo halijakuwa
na maendeleo mengi tangu Uhuru.
Wakenya pia waliikejeli kauli hiyo kupitia video fupi kwenye
TikTok wakiashiria kutoamini kama rais atatimiza ahadi hiyo.
Jumatano akiwajibu, Ruto alisema kwamba ameona baadhi ya
kejeli hizo akisema kwamba atatimiza ahadi ya kujenga barabara hiyo ya umbali
wa kilomita 750.
“Wiki mbili zilizopita
nilikuwa Kaskazini mashariki na nilitoa ahadi ya barabara ambayo itajengwa
kutoka Isiolo kupitia Wajir kuelekea Mandera. Na watu wengi wanadhani au
wanafikiria ni mzaha. Acha niwambieni watu wazuri, unajua katika taifa hili
baadhi wanachukulia suala la kufa na kupona kwa mzaha, nimejitolea kuhakikisha
barabara hiyo ya kilomita 750 kutoka Isiolo hadi Mandera kwa sababu kwa muda
mrefu tumekuwa tukitelekeza Kaskazini mashariki kimaendeleo,” Ruto alijibu.