logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Rais Ruto, Spika Kingi, Gavana Cheboi Wamuomboleza Seneta Cheptumo

RIP

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri16 February 2025 - 14:28

Muhtasari


  •  Cheptumo alifariki dunia katika Hospitali ya Nairobi siku ya Jumapili asubuhi wakati alipokuwa akipokea matibabu.
  •  Gavana wa Baringo, Benjamin Cheboi, alisema kifo cha Cheptumo ni pigo kubwa kwa kaunti hiyo na taifa kwa jumla.

Marehemu William Cheptumo

Rais William Ruto ameongoza taifa katika kuomboleza kifo cha Seneta wa Baringo, William Kipkorir Cheptumo.

 Cheptumo alifariki dunia katika Hospitali ya Nairobi siku ya Jumapili asubuhi wakati alipokuwa akipokea matibabu.

 Katika ujumbe wake wa rambirambi, Rais Ruto alimtaja marehemu kama kiongozi shupavu aliyejitolea kwa dhati katika utumishi wa umma.

 "Seneta William Cheptumo alikuwa kiongozi mwenye maono aliyekuwa na bidii katika kuhudumia wananchi. Alikuwa mchapakazi, mwenye sauti, na mtetezi wa maendeleo ya Baringo bila kuchoka. Familia ya Cheptumo, marafiki na wakazi wa Kaunti ya Baringo wako katika mawazo na maombi yetu. Pumzika kwa amani, Mheshimiwa," alisema Rais Ruto.

 Spika wa Seneti, Amason Kingi, naye alielezea huzuni yake kufuatia kifo cha ghafla cha Seneta Cheptumo, akisema kuwa ni pigo kubwa kwa Seneti na taifa kwa ujumla.

 "Seneti ya Kenya imepoteza kiongozi aliyekuwa muumini wa dhati wa ugatuzi. Cheptumo alijitahidi kuhakikisha kuwa mfumo wa ugatuzi unawanufaisha wananchi na alitetea maslahi yao bila woga. Namuomba Mwenyezi Mungu atujalie nguvu katika kipindi hiki kigumu," alisema Kingi.

 Kwa upande wake, Gavana wa Baringo, Benjamin Cheboi, alisema kuwa kifo cha Seneta Cheptumo ni pigo kubwa kwa kaunti hiyo na taifa kwa jumla.

 "Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Seneta wetu wa Baringo, Mheshimiwa William Cheptumo. Hili ni pigo kubwa kwetu sote. Rambirambi zangu kwa familia yake. Alikuwa kiongozi shupavu na rafiki wa dhati. Tutakutana kama viongozi wa Baringo, familia na marafiki ili kujadili hatua za mbele," alisema Gavana Cheboi.

Viongozi wengine wameendelea kutoa rambirambi zao kupitia vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii.

 Marehemu Cheptumo, aliyekuwa na umri wa miaka 57, alikuwa wakili kitaaluma na alihudumu kama Mbunge wa Baringo Kaskazini kati ya mwaka 2008 na 2013. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, alichaguliwa kuwa Seneta wa Baringo kupitia chama cha UDA, akimshinda Gideon Moi wa KANU.

 Katika Seneti, alihudumu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Kitaifa, Ulinzi na Masuala ya Kigeni, akionyesha uongozi wa hali ya juu katika masuala nyeti ya kitaifa.

 Kabla ya kujiunga na siasa, Cheptumo alifanya kazi kama afisa wa sheria katika Benki Kuu ya Kenya na Shirika la Maendeleo ya Viwanda na Biashara (ICDC). Pia alikuwa mwanzilishi wa kampuni ya uwakili ya Cheptumo and Company Advocates.

 Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika uongozi wa Baringo na Kenya kwa ujumla.

 Mwili wake umehifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya Lee Funeral huku mipango ya mazishi ikiendelea.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved