Youssouf alimshukuru Ruto kwa kumpongeza baada ya kushinda kiti cha mwenyekiti wa AUC katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi .
Youssouf alimtambua rais Ruto kama bingwa wa Afrika wa mageuzi na akaeleza kuwa yuko tayari kufanya kazi naye.
Mahmoud Ali Youssouf akizungumza na Rais William Ruto mnamo Februari 15, 2025.
Mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Mahmoud Ali Youssouf ametoa shukrani zake kwa Rais wa Kenya William Ruto.
Katika taarifa yake Jumapili asubuhi, Youssouf alimshukuru Ruto kwa kumpongeza baada ya kushinda kiti cha mwenyekiti wa AUC katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi Februari 15, 2025.
Waziri huyo wa zamani wa maswala ya kigeni wa Djibouti alimtambua rais Ruto kama bingwa wa Afrika wa mageuzi na akaeleza kuwa yuko tayari kufanya kazi naye.
"Asante HE rais William Ruto kwa kunipongeza kwa ushindi wangu," Youssouf alisema kupitia X.
"Yeye ndiye bingwa wa Afrika wa Mageuzi: Nina heshima kufanya kazi naye kuendeleza ajenda yetu ya bara : Asanti sana Mzee," aliongeza.
Katika uchaguzi huo, Youssouf alishinda baada ya kupata kura zinazohitajika katika raundi ya saba, ambapo alikuwa mgombea pekee baada ya mgombea wa Kenya RailaOdinga kuondolewa katika raundi ya sita.
Richard Randriamandrato wa Madagascar aliondolewa mapema baada ya kushika mkia katika awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na ya nne na kuwaacha Raila na Youssof kumenyana.
Youssouf alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 33 zilizohitajika katika raundi ya saba ya upigaji kura, ambayo alishinda peke yake.
Jumamosi jioni, Rais Ruto alituma ujumbe wa faraja kwa Raila Odinga baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Katika taarifa yake, Ruto amepongeza juhudi za Odinga na kushukuru uongozi wa bara Afrika kwa kutilia maanani maono yake kwa Umoja wa Afrika.
Licha ya kufurahia kuungwa mkono na mataifa yasiyopungua ishirini, Raila alishindwa na Mahmoud Youssouf wa Djibouti katika uchaguzi huo wa Jumamosi jioni baada ya raundi saba za upigaji kura.
"Ingawa matokeo ya uchaguzi huu hayakumfaa mgombea wa Kenya, ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa bara letu. Asanteni kwa kuzingatia maono na vipaumbele vya Mheshimiwa Raila Odinga kwa Umoja wa Afrika na kumpa nafasi ya kushiriki shauku yake kwa mageuzi ya bara hili," alisema Ruto katika taarifa.
Aidha, Rais Ruto aliwapongeza Mahmoud Youssouf na Selma Haddadi kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti wa AUC, akiwahakikishia kuwa Kenya itawaunga mkono kikamilifu katika uongozi wao.
"Uchaguzi huu haukuwa kuhusu mtu binafsi au taifa fulani, bali mustakabali wa Afrika. Mustakabali huo ungali na matumaini, na kwa pamoja tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya Afrika iliyoungana, iliyo na ustawi, na yenye ushawishi mkubwa katika jukwaa la kimataifa," aliongeza.