Raila amekubali matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa AUC baada ya kushindwa na Mahamoud Ali Youssouf.
Raila alimtakia kila la heri Youssouf akimpongeza kwa kupata ridhaa ya viongozi wa Afrika kuongoza Umoja wa Afrika.
Waziri Mkuu wa Zamani Raila Amollo Odinga
Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, amekubali matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) baada ya kushindwa na Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti.
Akizungumza na wanahabari Jumamosi jioni baada ya uchaguzi huo uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Raila alisema kuwa demokrasia ilizingatiwa kikamilifu na akampongeza mshindi.
“Ninakubali matokeo ya kura. Kwa hivyo, ninakubali kushindwa,” alisema Raila, akisisitiza kuwa uchaguzi huo ni mfano wa kuimarisha demokrasia barani Afrika.
Alieleza kuwa alikuwa tayari kwa matokeo yoyote na kwamba hana kinyongo na uamuzi wa wakuu wa mataifa ya Umoja wa Afrika.
Licha ya kushindwa, Raila alisisitiza kuwa bado yuko tayari kuendelea kutoa mchango wake kwa maendeleo ya bara la Afrika katika nyanja nyingine.
"Sina uchungu. Kwa kweli, nina furaha na niko tayari kutoa huduma zangu kwa bara hili kwa njia yoyote ile," alisema.
Kiongozi huyo wa ODM aliongeza kuwa alitimiza wajibu wake kama mgombea kwa kukutana na viongozi mbalimbali wa Afrika na kushiriki maono yake kwa AUC.
Katika hotuba yake, Raila alitoa shukrani kwa wale waliompigia kura pamoja na wale waliompigia mpinzani wake, akisema wote walitekeleza haki yao ya kidemokrasia.
“Ninawashukuru wale waliopiga kura kwa kunichagua. Pia nawapongeza waliompigia mwenzangu kwa kuwa walitumia haki yao ya kidemokrasia,” alisema.
Raila alimtakia kila la heri mshindi, Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti, akimpongeza kwa kupata ridhaa ya viongozi wa Afrika kuongoza Umoja wa Afrika.
“Namtakia mpinzani wangu kila la heri. Namtakia mafanikio katika majukumu yake mapya,” alisema.
Baada ya kushindwa kutwaa kiti hicho, Raila alisema atarejea Kenya kuendelea na shughuli nyingine, akibainisha kuwa kuna mambo mengi yanayohitaji kushughulikiwa.
"Sasa mpango wangu ni kurudi nyumbani kwa sababu kuna mambo mengi ya kushughulikia," alisema.
Katika uchaguzi huo, Youssouf alishinda baada ya kupata kura zinazohitajika katika raundi ya saba, ambapo alikuwa mgombea pekee baada ya Raila kuondolewa katika raundi ya sita.
Richard Randriamandrato wa Madagascar aliondolewa mapema baada ya kushika mkia katika awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na ya nne na kuwaacha Raila na Youssof kumenyana.
Youssouf alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 33 zilizohitajika katika raundi ya saba ya upigaji kura, ambayo alishinda peke yake.