Ruto, ametuma ujumbe wa faraja kwa Raila Odinga baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa AUC.
Ruto pia aliwapongeza Mahmoud Youssouf na Selma Haddadi kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti wa AUC.
Raila Odinga na Rais William Ruto wakiwa Homa Bay
Rais wa Kenya, William Ruto, ametuma ujumbe wa faraja kwa Raila Odinga baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Katika taarifa yake, Ruto amepongeza juhudi za Odinga na kushukuru uongozi wa bara Afrika kwa kutilia maanani maono yake kwa Umoja wa Afrika.
Licha ya kufurahia kuungwa mkono na mataifa yasiyopungua ishirini, Raila alishindwa na Mahmoud Youssouf wa Djibouti katika uchaguzi huo wa Jumamosi jioni baada ya raundi saba za upigaji kura.
"Ingawa matokeo ya uchaguzi huu hayakumfaa mgombea wa Kenya, ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa bara letu. Asanteni kwa kuzingatia maono na vipaumbele vya Mheshimiwa Raila Odinga kwa Umoja wa Afrika na kumpa nafasi ya kushiriki shauku yake kwa mageuzi ya bara hili," alisema Ruto katika taarifa.
Aidha, Rais Ruto aliwapongeza Mahmoud Youssouf na Selma Haddadi kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti wa AUC, akiwahakikishia kuwa Kenya itawaunga mkono kikamilifu katika uongozi wao.
"Uchaguzi huu haukuwa kuhusu mtu binafsi au taifa fulani, bali mustakabali wa Afrika. Mustakabali huo ungali na matumaini, na kwa pamoja tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya Afrika iliyoungana, iliyo na ustawi, na yenye ushawishi mkubwa katika jukwaa la kimataifa," aliongeza.
Taarifa hii inajiri baada ya Raila Odinga kushindwa katika kinyang’anyiro cha kuiongoza AUC, uchaguzi uliovuta hisia na kufuatiliwa kwa karibu na mataifa mbalimbali barani Afrika.
Raila aliondolewa kwenye uchaguzi huowa Jumamosi baada ya kupoteza kwa Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti katika awamu ya tano na sita ya upigaji kura.
Richard Randriamandrato wa Madagascar aliondolewa mapema baada ya kushika mkia katika awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na ya nne na kuwaacha Raila na Youssof kumenyana.
Youssouf alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 33 zilizohitajika katika raundi ya saba ya upigaji kura, ambayo alishinda peke yake.
Katika taarifa tofauti, Naibu Rais Kithure Kindiki alisema Rais na Raila na timu yake ya kampeni walijitolea kwa uwezo wao lakini kwa bahati mbaya wakapoteza.
"Tunasalia kuwa taifa la kujivunia kwamba tulikaribia sana. Leo haikuwa siku yetu, siku yetu itafika. Shukrani kwa marafiki wote wa Kenya ambao walisimama nasi wakati muhimu," Kindiki alisema.