
Taifa la Kenya limeingia katika maombolezo kufuatia kifo cha Mbunge wa Malava, Mheshimiwa Moses Malulu Injendi. Mbunge huyo alifariki Jumatatu akipokea matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.
Kufuatia msiba huo, viongozi wa ngazi za juu nchini wakiongozwa na Rais William Ruto, Naibu Rais Kithure Kindiki, na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wameeleza huzuni yao kwa kumpoteza ambaye wametaja kuwa kiongozi shupavu na mwakilishi wa wananchi aliyejitolea kwa dhati.
Rais Ruto, katika rambirambi zake, alimtaja Malulu Injendi kama kiongozi mwenye dira aliyewahudumia wananchi wa Malava kwa kujitolea.
"Nimehuzunishwa sana na kifo cha rafiki na mwenzangu, Mheshimiwa Malulu Injendi. Alikuwa kiongozi mwenye msimamo thabiti aliyewatumikia wananchi wake kwa uaminifu na uadilifu. Alijitahidi kuhakikisha kuwa fursa za elimu zinapatikana kwa wote. Tunawaombea faraja familia yake, marafiki na watu wa Malava katika kipindi hiki kigumu. Pumzika kwa amani, rafiki yangu," alisema Rais Ruto.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, alieleza masikitiko
yake kwa kumpoteza kiongozi aliyekuwa rafiki wa wengi na mzalendo wa kweli.
"Kifo kimetunyang’anya kiongozi mahiri na rafiki wa wengi. Tunawaombea neema na amani familia yake pamoja na wananchi wa Malava katika kipindi hiki cha majonzi," alisema Kindiki.
Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alimtaja Injendi kama mtu mtulivu na mwenye kujali maslahi ya jamii yake.
"Mheshimiwa Malulu Injendi alikuwa kiongozi makini na mcha Mungu. Alikuwa rafiki yangu wa karibu wakati tulipohudumu pamoja katika Bunge la 12. Kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa familia yake, watu wa Malava, na jamii ya eneo la Magharibi mwa Kenya. Nawapa pole za dhati familia yake na watu wa Malava. Mungu ampumzishe kwa amani," alisema Gachagua.
Malulu Injendi alihudumu kama Mbunge wa Malava kwa muhula wake wa tatu mfululizo tangu 2013. Aidha, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Elimu na Utafiti, ambapo alijitahidi kuboresha sekta ya elimu nchini.
Bunge la Kitaifa linatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha mbunge huyo, huku familia na viongozi wa kisiasa wakiendelea kuomboleza msiba huo mzito.