
SENETA wa Nandi Samson Cherargei ametetea mswada wake unaolenga kuongezwa kwa muda wa muhula wa kuhudumu kwa rais kutoka kwa miaka 5 hadi 7.
Akizungumza katika mazungumzo na kituo kimoja cha redio humu
nchini, mwandani huyo wa rais William Ruto alisema kwamba kando na kipindi
hicho kumpa rais muda zaidi wa kufanya kazi na kutimiza ahadi zake kwa wapiga
kura, pia nambari 7 kwa Wakristo ina umuhimu mkubwa.
“Jambo la kwanza unajua
nambari 7 ni nambari takatifu kwetu sisi ambao ni Wakristo. Jambo la pili
nimeshawaambia kwamba hili taifa limekuwa ni la kisiasa kwa muda wote, ni nadra
sana kiongozi kupata muda wa kutosha wa kutekeleza majukumu yake,” Cherargei alieleza.
Cherargei Alifichua kwamba kila mtu nchini Kenya amekuwa
akiendesha siasa za kampeni tangu mwaka 2022 uchaguzi ulipokamilika.
Kulingana na seneta huyo, Kenya inastahili kuwa na sheria kama
ya jirani Tanzania ambapo kuna sheria kali inayozuia kampeni za siasa nje ya
kipindi cha mwaka au miezi 6 kabla ya uchaguzi mkuu.
“Kuna rafiki yangu kutoka
Tanzania alikuwa ananiambia katika sheria yao, ukiendesha kampeni nje ya mwaka
mmoja au mwaka mmoja kabla ya uchaguzi unakamatwa na kushtakiwa. Lakini hapa
Kenya watu wataanza kusema ni hujumu ya kidemokrasia,” Cherargei alisema.
Seneta huyo alitangaza kuwasilisha mswada huo mwaka jana
ambapo analenga muhula wa kisiasa kuongezwa kutoka miaka 5 kama ilivyo kwa sasa
chini ya katiba ya 2010, hadi miaka 7.
Hata hivyo, ni mswada ambao ulipokea maoni mengi ya kuupinga,
japo seneta Cherargei bado anaonekana kuwa na azma ya kuufufua na kuuwasilisha
bungeni.