
SENETA wa Nandi, Samson Cherargei amewakashifu baadhi ya Wakenya wanaosherehekea kushindwa kwa Raila Odinga kwenye AUC.
Akizungumza katika kikao cha bunge la seneti Alhamisi,
Cherargei alimpongeza Odinga kwa kustahimili kinyang’anyiro hicho kikali kuanzia
kampeni hadi shughuli nzima ya upigani kura.
Cherargei alisema kwamba Odinga katika umri wake – 80 –
alijaribu sana kustahimili hadi raundi ya 6 ambapo aliamua kujiondoa na
kumuacha mgombea mwenza Mahmoud Youssouf kushinda katika raundi ya 7 kwa kura
33.
“Ningependa kushukuru
mataifa 22 kutoka kwa umoja wa Afrika ambao walisimama na Raila Odinga kwa
raundi 7. Raila Odinga alishinda raundi mbili na si rahisi kuenda raundi 7,
tunajua watu ambao wanaenda kwa dakika 1 na sekunde 59 lakini katika umri wake,
Baba Raila alijaribu kusimama kwa raundi 7 katika uchaguzi wa AUC,” Cherargei alisema.
“Kwa hivyo tunamsherehekea na kukubali chenye alifanya, raundi 7 katika umri wake sio jambo rahisi kwenye kinyang’anyiro cha AUC,” aliongeza.
Hata hivyo, Radio Jambo inaweza kuripoti kwamba Raila Odinga
alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho katika raundi ya 6 baada ya kupata kura
22 dhidi ya 26 za Youssouf kutoka Djibout.
Mgombea huyo wa Djibout alishinda katika raundi ya 7 ambayo
alikuwa peke yake ambapo alihitajika kufikisha akidi hitajika ya kura 33 sawa
na thuluthi mbili za kura.
Youssouf aliapishwa kama mwenyekiti mpya wa AUC ambaye
alimrithi Moussa Faki.