
Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya (EU), Ursula von der Leyen, amempongeza Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Kupitia ujumbe wake kwenye ukurasa rasmi wa X, von der Leyen alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika (AU), akieleza matumaini yake ya kuimarisha uhusiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.
"Hongera kwa Rais @ymahmoudali kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tume ya Umoja wa Afrika. Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wana ushirikiano imara, na ninatarajia kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na changamoto za pamoja na kusongesha malengo yetu ya pamoja," alisema von der Leyen siku ya Jumapili.
Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wamekuwa na uhusiano wa muda mrefu unaojikita katika nyanja mbalimbali, ikiwemo maendeleo ya kiuchumi, usalama, elimu, na mabadiliko ya tabianchi.
EU imekuwa mshirika mkuu wa AU katika kusaidia miradi ya maendeleo barani Afrika, ikitoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa nchi wanachama wa AU.
Kwa pongezi zake, Ursula von der Leyen ameonyesha dhamira ya Umoja wa Ulaya kuendelea kushirikiana na AU ili kuleta maendeleo na utulivu barani Afrika.
Mataifa wanachama wa AU na EU sasa yanaangazia mustakabali wa ushirikiano huu chini ya uongozi mpya wa Youssouf, huku matarajio yakiwa ni kuimarisha mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya ustawi wa wote.
Katika uchaguzi wa siku ya Jumamosi, Youssouf alishinda baada ya kupata kura zinazohitajika katika raundi ya saba, ambapo alikuwa mgombea pekee baada ya mgombea wa Kenya RailaOdinga kuondolewa katika raundi ya sita.
Richard Randriamandrato wa Madagascar aliondolewa mapema baada ya kushika mkia katika awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na ya nne na kuwaacha Raila na Youssof kumenyana.
Youssouf alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 33 zilizohitajika katika raundi ya saba ya upigaji kura, ambayo alishinda peke yake.