Gachagua, amempongeza Raila kwa juhudi zake katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.
Gachagua amesisitiza kuwa Raila hakushindwa, bali ni demokrasia iliyoshinda kwa kuwa walio wengi waliamua.
Rigathi Gachagua amempongeza Raila Odinga
Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, amempongeza Raila Odinga kwa juhudi zake katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), akimtaja kama shujaa aliyeonyesha uthabiti na nguvu za uongozi barani Afrika.
Katika ujumbe wake kwa Raila baada ya kushika nafasi ya pili katika uchaguzi huo uliofanyika Februari 15, Gachagua alisema kuwa ingawa Raila hakushinda kiti hicho, alibeba bendera ya Kenya kwa heshima na kufanya taifa kujivunia.
"Baba Raila Odinga, umeonyesha moyo wa uthabiti, ari, na nguvu zisizochoka za Simba wa Afrika. Uliibuka wa pili kwa heshima kubwa katika kinyang'anyiro kikali cha uongozi wa AUC," aliandika Gachagua siku ya Jumapili adhuhuri.
Gachagua alisisitiza kuwa Raila hakushindwa, bali ni demokrasia iliyoshinda kwa kuwa walio wengi waliamua.
Alimpongeza kwa hatua aliyopiga, akisema kuwa juhudi zake zilionyesha matumaini makubwa kwa Kenya, Afrika, na dunia kwa ujumla.
"Afrika ilikuwa na uhitaji mkubwa wa uongozi wako, lakini kwa hekima ya Mungu, inaonekana kuwa bado kuna jukumu kubwa linalokusubiri hapa nyumbani. Wewe ni mwana wa Kenya, na ndugu zako bado wanakuhitaji katika safari ya kulikomboa taifa letu dhidi ya uongozi wa kizembe," alisema.
Licha ya matokeo hayo, Gachagua alisema kuwa uchaguzi wa AU haupunguzi hadhi ya uongozi wa Raila wala azma yake ya kutafuta suluhu kwa changamoto zinazolikabili taifa la Kenya.
"Karibu nyumbani mwana wetu Raila Odinga, ukiwa na kichwa chako kikiwa juu. Mashariki au Magharibi, nyumbani ni nyumbani. Jipe moyo, umeifanyia Kenya fahari," alihitimisha.
Raila alikuwa mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo ya juu katika Umoja wa Afrika lakini alishindwa na mshindani wake mkuu, Mahmoud Ali Youssouf kutoka Djibouti, aliyeungwa mkono na idadi kubwa ya nchi wanachama.
Katika uchaguzi huo, Youssouf alishinda baada ya kupata kura zinazohitajika katika raundi ya saba, ambapo alikuwa mgombea pekee baada ya mgombea wa Kenya RailaOdinga kuondolewa katika raundi ya sita.
Richard Randriamandrato wa Madagascar aliondolewa mapema baada ya kushika mkia katika awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na ya nne na kuwaacha Raila na Youssof kumenyana.
Youssouf alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 33 zilizohitajika katika raundi ya saba ya upigaji kura, ambayo alishinda peke yake.