
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ametuma salamu za pongezi kwa Mahmoud Ali Youssouf baada ya kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) katika Mkutano wa 38 wa Umoja wa Afrika.
Kupitia taarifa rasmi, Museveni pia alimpongeza Selma Malika Haddadi kwa kushinda nafasi ya Naibu Mwenyekiti wa Tume hiyo, akieleza kuwa Uganda inasalia kuwa mshirika mwaminifu wa Umoja wa Afrika katika juhudi za kutatua changamoto za bara hili na kutumia fursa zilizopo kwa manufaa ya wananchi wake.
"Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Uganda, na kwa niaba yangu binafsi, ninatoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Mahmoud Ali Youssouf na Selma Malika Haddadi kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika mtawalia katika Mkutano wa 38 wa AU," alisema Museveni.
Aidha, Rais Museveni alisisitiza dhamira ya Uganda kushirikiana kwa karibu na Tume ya Umoja wa Afrika ili kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazolikumba bara la Afrika na kuboresha hali ya maisha ya raia wake.
Uchaguzi wa viongozi wa Tume ya Umoja wa Afrika huwa unafanyika kila baada ya miaka minne, na viongozi wapya wanatarajiwa kusimamia ajenda ya maendeleo ya bara hili, kushughulikia masuala ya usalama, diplomasia, na ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa wanachama wa AU.
Mahmoud Ali Youssouf, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, atachukua nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne, akiongoza juhudi za kuimarisha mshikamano wa bara la Afrika katika nyanja mbalimbali.
Katika uchaguzi wa Jumamosi, Februari 16, Youssouf alishinda baada ya kupata kura zinazohitajika katika raundi ya saba, ambapo alikuwa mgombea pekee baada ya mgombea wa Kenya RailaOdinga kuondolewa katika raundi ya sita.
Richard Randriamandrato wa Madagascar aliondolewa mapema baada ya kushika mkia katika awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu na ya nne na kuwaacha Raila na Youssof kumenyana.
Youssouf alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 33 zilizohitajika katika raundi ya saba ya upigaji kura, ambayo alishinda peke yake.