
JUMUIYA ya watu wasioamini katika uwepo wa Mungu nchini Kenya wamepongeza viongozi wa mataifa ya Afrika kwa kutomchagua aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa AUC kutoka Kenya.
Wakizungumza kupitia chapisho kwenye kurasa zao za mitandao ya
kijamii, Jumuiya hiyo inayoongozwa na Harrison Mumia ilisema kwamba kama kuna
jambo la muhimu marais wa takriban mataifa 50 ya Afrika walifanya basi ni
kutomchagua Raila Odinga.
Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, Odinga alipaswa kufeli katika
kinyang’anyiro hicho kwani alishachafua jina lake zuri alilolijenga kwa muda
mrefu kuhusu kupigania haki za kibinadamu, pale alipoamua kujihusisha na
serikali ya rais Ruto.
Jumuiya ilisema kwamba
serikali ya Kenya chini ya rais William Ruto imejizolea umaarufu katika mauaji
na utekaji nyara, hivyo Raila kushirikiana nayo ni sawa na kupaka damu jina
lake.
“Siku ya Jumamosi, Raila
Odinga alishindwa vilivyo na mgombea wa Djibouti, Ali Youssouf, katika uchaguzi
wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika. Tunatoa pongezi zetu kwa Ali Youssouf
na tunamtakia kila la kheri katika jukumu lake jipya.”
“Raila Odinga
amewaangusha wananchi wa Kenya kwa kuachia wadhifa wake wa kiongozi wa upinzani,
na kuunda muungano wa hila na Rais William Ruto. Inasikitisha kwamba, baada ya
kujijengea taswira ya kuwa mtetezi wa haki za binadamu na uzingatiaji wa
katiba, ameungana na serikali ambayo imekuwa maarufu kwa utekaji nyara, na
utawala mbovu.”
“Kutokana na hali hiyo,
tunaamini kuwa viongozi wa Afrika walifanya uamuzi wa busara kumnyima
uenyekiti. Ni wakati wa Raila kujitenga na kuruhusu Wakenya kujiamulia
mustakabali wao wenyewe,” jumuiya hiyo ilichapisha.
Raila Odinga alijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho katika
raundi ya 6 baada ya kujizolea kura 22 dhisdi ya 26 za Mahmoud Ali Youssouf kutoka
Djibout.
Mgombea huyo wa Djibout alikwenda katika raundi ya 7 peke
yake na kujizolea kura 33, ambazo ni thuluthi mbili iliyostahiki kupata
mshindi.
Youssouf sasa ndiye mwenyekiti mpya wa tume ya Afrika ambaye
amechukua uongozi kutoka kwa mwenyekiti anayeondoka, Moussa Faki.