
Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua amemtaja Rais William Ruto kuwa msaliti na mnafiki mkubwa.
Akizungumza katika mji wa Maua, Kaunti ya Meru, siku ya Jumamosi, Juni 21, 2025, Gachagua alisema Rais alimfuta kazi Mithika Linturi hata baada ya waziri huyo wa zamani kumpa mahali pa kulala.
Gachagua alisema Ruto aliwadanganya watu wa eneo hilo kwa kujifanya kuwa mtu wa imani, ilhali alikuwa akijificha kama mnyama.
“William Ruto alitudanganya. Alikuja na Biblia na kusema ameokoka, lakini alikuwa fisi aliyevaa ngozi ya kondoo. Ni nani alimfukuza Linturi?” Gachagua aliuliza umati.

“Nikuulize William Ruto. Unakuja hapa Maua, unalala kwa nyumba ya Linturi, unalala kitandani mwake, unakula chakula chake, unakunywa maji yake, halafu unamgeuka na kumfukuza. Wewe si mnyama? Ruto si mnyama?”
“Mtu anakukaribisha nyumbani kwake, anakulisha, unalala, unatumia choo chake, halafu unamsaliti?”
Gachagua aliendelea kusema kuwa sasa ameungana na Linturi, na wanaunda ushirikiano wa kisiasa pamoja na viongozi wa upinzani.
“Linturi na mimi tumepanga. Huyu Kasongo naye ana mipango yake. Tumeungana na Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Martha Karua na Fred Matiang’i.
"Tumekubaliana kuwa siku za usoni tutaungana, tutatoa kiongozi mmoja kupambana na Kasongo,” alitangaza.
Mithika Linturi alitimuliwa kufuatia kashfa ya mbolea ya mwaka 2024 iliyotikisa Wizara ya Kilimo.
Ingawa Ruto alidai kuwa hatua hiyo ilikuwa kwa ajili ya uwajibikaji, wandani wa Linturi akiwemo Gachagua wanaamini kuwa ilikuwa na nia ya kisiasa.
Naibu Rais wa zamani sasa anajitokeza kama mtetezi wa maslahi ya Wakenya, hata akiwatafuta viongozi wa upinzani kuunda muungano wa pamoja dhidi ya kile anachokiita usaliti wa Ruto.

Kauli za Gachagua zinaashiria mikakati mipya ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, ambapo waliokuwa mahasimu sasa wanaungana kumpinga rais aliye madarakani.