
Kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, amedai kuwa Kithure Kindiki aliwalipa Wabunge kutoka Kaunti ya Meru hadi shilingi milioni tano kila mmoja ili kumzuia kuandaa mikutano ya kisiasa katika eneo hilo.
Akizungumza Jumapili, Juni 22, 2025, katika ibada ya kanisa la AIPCA ST. Mary’s, eneo bunge la Buuri, Kaunti ya Meru, Gachagua alisema kuwa wandani wa Rais William Ruto walikumbwa na wasiwasi baada ya mapokezi makubwa aliyopata katika ziara yake ya siku tatu kaunti hiyo.
“Tumekuwa hapa Meru nyumbani, the land of my mother, na tumefurahi sana. Huyu Ruto alikuwa amesema tusikanyage Meru,” alisema Gachagua.
Gachagua alidai kuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake huko Imenti, wabunge wa eneo hilo walipatiwa shilingi milioni mbili kila mmoja na Kindiki ili kuwaajiri vijana kuvuruga mikutano yake.
“Wale wabunge wakapatiwa na yule mtu wa soprano shilingi milioni mbili watafute vijana watupige mawe tusiende kwa mikutano,” alisema.
Hata hivyo, badala ya kuwa na vurugu, Gachagua alisema kuwa vijana hao walihudhuria mikutano yake na kuanza kuimba kauli ya “one term.”
“Wale vijana waliokuwa wamepewa pesa Nkubu na Meru Tuskys, kuona mimi wakaanza kuimba ‘one term’, wakaingia kwa mkutano wangu,” alieleza.
Gachagua alisema kuwa baada ya uungwaji mkono huo wa kushangaza, kundi la Ruto lilikumbwa na hofu.
Alidai kuwa Kindiki aliitisha kikao cha dharura usiku huo na wabunge kutoka Igembe na maeneo mengine, na kuwahimiza kuhakikisha Gachagua hakanyagi maeneo yao.
“Sasa ndiye huyu mtu wa soprano akapanick usiku mzima ni kukaza wajumbe wa Igembe, huyu mtu asikubaliwe kukanyaga Igembe,” alisema Gachagua.
Aliendelea kudai kuwa wabunge hao walitumia fursa hiyo kuomba fedha zaidi, wakisema mgao wa awali haukutosha kukabiliana na umaarufu wake unaokua.
“Ile pesa ya budget ulitupatia haitoshi. Utuongezee milioni mbili,” alisema.
Kwa mujibu wa Gachagua, wabunge wa Tigania Mashariki, Igembe Kati, Igembe Kaskazini na hata Kusini walipewa kila mmoja shilingi milioni tano kwa masharti ya kumzuia kuzungumza katika kaunti hiyo.
“Na wakaassure William Ruto as long as you are in Meru County, huyo mkabila hatakubaliwa kuongea ata na watu kumi hii county,” alidai.
Kauli hizo zinaangazia mvutano unaozidi kuongezeka kati ya Gachagua na aliyekuwa bosi wake, Rais Ruto, kuelekea uchaguzi wa 2027.
Gachagua, ambaye sasa yuko upande wa upinzani chini ya chama cha DCP, ameendeleza kampeni za nguvu za mashinani katika eneo la Mlima Kenya Mashariki, akimtishia moja kwa moja Rais Ruto katika ngome yake ya kisiasa.