
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu almaarufu Bobi Wine amekashifu kauli ya Rais Yoweri Museveni kuhusu kuzuiliwa kwa mwanasiasa mkongwe Kizza Besigye na hali yake ya afya kuwa ambayo imezorota.
Siku ya Jumanne, Museveni alitoa taarifa ndefu akitaka kesi dhidi ya mpinzani huyo wake wa muda mrefu kuharakishwa na akaeleza kuwa matatizo yake ya kiafya yanatokana na mgomo wake wa kula.
Akizungumza kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii Jumanne jioni, Bobi Wine hata hivyo alikosoa wito wa Museveni wa kuharakishwa kwa kesi ya Besigye akimtaja kuwa mnafiki.
Kiongozi huyo wa chama cha National Unity Platform (NUP) aliendelea kudai kuachiliwa mara moja kwa Besigye pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa.
"Dikteta muovu, asiye na aibu na mnafiki anasema kwa urahisi kwamba Dk. Besigye alipaswa kudai kesi ya haraka badala ya kugoma kula ili kupinga kuendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria. Anaongeza kuwa mahakama ya kijeshi ilikuwa tayari kuendesha kesi (haramu)!
Hata hivyo, ni Museveni huyo huyo ambaye amehakikisha kwamba wafuasi wa NUP wanakaa MIAKA MINNE kizuizini bila kufunguliwa mashtaka. Miaka minne! Wakati wote huu, hakuna ushahidi wowote ulioletwa dhidi ya vijana hawa, hakuna shahidi wa kuwabana kwa kosa lolote. Badala yake, watendaji wake wamekuwa wakiwatembelea ili kuwalazimisha kukiri makosa ambayo hawakufanya kwa ahadi za pesa na kazi. Kwa hiyo anazungumzia kesi gani ya haraka?!,” Bobi Wine aliandika.
Aliongeza, “Madai yetu bado yapo. Huru Dk. @kizzabesigye1 na wafungwa wengine wa kisiasa!”
Katika taarifa aliyotoa kwa umma siku ya Jumanne, Museveni alieleza kuwa Besigye ameshikiliwa kwa tuhuma nzito zinazohusiana na usalama wa taifa.
Alisema badala ya wananchi kuhoji kwa nini Besigye amezuiliwa kwa muda mrefu, wanapaswa kuzingatia sababu ya kukamatwa kwake na umuhimu wa kusikilizwa kwa kesi hiyo haraka.
"Ikiwa unataka nchi tulivu, swali sahihi linapaswa kuwa: ‘Kwa nini Dkt. Besigye amekamatwa?’ Jawabu sahihi ni kuwa na kesi ya haraka ili ukweli uweze kufahamika. Vinginevyo, tunahatarisha usalama wa nchi, jambo ambalo ni hatari sana," alisema Museveni.
Kizza Besigye, ambaye amekuwa mpinzani wa muda mrefu wa Museveni tangu miaka ya 2000, amekamatwa mara kadhaa kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo uchochezi na kuandaa maandamano dhidi ya serikali.
Mwaka 2005, alikamatwa kwa tuhuma za uhaini na ubakaji, ingawa baadaye aliachiliwa kwa dhamana. Katika miaka ya hivi majuzi, amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Museveni, akipinga kile anachokiita udikteta na ukandamizaji wa haki za raia.
Museveni amekosoa wale wanaotaka Besigye aachiliwe kwa msamaha au dhamana, akisema kuwa mtazamo wa serikali yake ni kuhakikisha uwajibikaji kwa wote wanaovuruga usalama wa nchi.
Kuhusu kucheleweshwa kwa kesi ya Besigye, Museveni alieleza kuwa Mahakama za Kijeshi ziliona dosari katika ushahidi na kuamuru kesi ihamishiwe Mahakama za Kiraia. Alisema serikali na wabunge wanashughulikia marekebisho ya kisheria ili kuziba mianya hiyo na kuharakisha kesi za aina hii siku za usoni.
"Mahakama za Kijeshi zilikuwa tayari kwa kesi hiyo, lakini zilibaini baadhi ya mapungufu na kuamuru kesi ihamishiwe Mahakama za Kiraia. Hili ndilo limesababisha kucheleweshwa kwa mchakato," alifafanua Museveni.
Kuhusu hali ya afya ya Besigye, Museveni alisema kuna hospitali ya serikali ndani ya gereza, na kwamba madaktari wake binafsi wamekuwa wakimtembelea na hata kumpeleka kwenye kliniki binafsi kwa matibabu. Aliongeza kuwa iwapo kutahitajika matibabu zaidi, serikali iko tayari kutoa huduma hiyo.
Hata hivyo, Museveni alidai kuwa udhaifu wa Besigye unahusiana zaidi na mgomo wake wa kula, ambao alitaja kama jaribio la kushinikiza mahakama kuwa na huruma badala ya kusubiri kesi kusikilizwa.
"Kama mtu hana hatia, kwa nini hapiganii kesi ya haraka kuthibitisha hilo, badala ya mgomo wa kula ili kupata huruma ya kupewa dhamana?" alihoji Museveni.
Besigye aliripotiwa kuanza mgomo wa kula akiwa gerezani kama njia ya kupinga kizuizini chake.
Picha zake zilisambaa kwenye vyombo vya habari zikimuonyesha akiwa dhaifu, hali iliyozua mjadala mkubwa kuhusu afya yake. Hata hivyo, serikali inasisitiza kuwa hatua yake ni mbinu ya kisiasa ya kujipatia huruma ya umma.
Museveni alihitimisha kwa kusema kuwa kesi ya Besigye inapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, na kwamba serikali haitaruhusu upotoshaji wa ukweli kwa manufaa ya kisiasa.