logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Bobi Wine Afichua Jinsi Kizza Besigye Alidhoofika Kutokana Na Kususia Chakula, Adai Aachiliwe

Bobi Wine ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya afya ya mwanasiasa mkongwe Dkt. Kizza Besigye.

image
na Samuel Mainajournalist

Kimataifa17 February 2025 - 13:05

Muhtasari


  • Bobi ameeleza kuwa hali ya Besigye imedhoofika sana baada ya kugoma kula akipinga kile anachokitaja kama kizuizi chake kisicho halali.
  • Hali hii inaendelea kuzua wasiwasi kuhusu ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa nchini Uganda.

Bobi Wine na Kizza Besigye

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Robert Kyagulanyi almaarufu kama Bobi Wine, ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya afya ya mwanasiasa mkongwe Dkt. Kizza Besigye.

Katika taarifa aliyotoa Jumatatu asubuhi, Bobi alieleza kuwa hali ya Besigye imedhoofika sana baada ya kugoma kula akipinga kile anachokitaja kama kizuizi chake kisicho halali.

Kiongozi huyo wa chama cha National Unity Platform (NUP) alieleza kuwa yeye na wenzake walitembelea Gereza la Luzira Upper kwa lengo la kumwona Dkt. Besigye, lakini hawakufanikiwa kumwona kutokana na udhaifu mkubwa alionao.

"Tulipitia Luzira Upper Prison kumtembelea Dkt. Kizza Besigye, lakini hatukuweza kumuona kwa sababu amedhoofika sana. Alituma ujumbe kwetu kupitia Hajj Obed Lutale Kamulegeya, aliyetufahamisha kuhusu hali yake ya afya inayotia wasiwasi, hadi kufikia hatua ya kuzimia asubuhi ya leo," alisema Bobi Wine.

Dkt. Besigye, ambaye amekuwa kiongozi wa upinzani nchini Uganda kwa muda mrefu anasisitiza kuwa anapaswa kuachiliwa huru, na ikiwa serikali ina kesi yoyote halali dhidi yake, basi inapaswa kufikishwa mbele ya mahakama ya kiraia.

Mbali na Dkt. Besigye, Bobi Wine na wenzake pia walikutana na mwanaharakati Bobi Young, ambaye aliwatumia salamu kwa wananchi wote.

Aidha, Bobi Wine alibainisha kuwa baadaye Jumatatu watafanya mkutano na wanaharakati wenzao kutoka vuguvugu nyingine za mageuzi kujadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kushinikiza kuachiliwa kwa Dkt. Besigye na wafungwa wengine wa kisiasa.

"Kwa sasa, tunatoa wito kwa wananchi wote kuchukua hatua zozote zinazowezekana kudai uhuru wao," alihitimisha Bobi Wine.

Hali hii inaendelea kuzua wasiwasi kuhusu ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa nchini Uganda, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakisihi serikali kuheshimu misingi ya haki na demokrasia.

Haya yanajiri saa chache baada ya Besigye kuripotiwa kukimbizwa hospitalini akiwa katika hali mahututi.

Mnamo siku ya Jumapili, mpinzani huyo wa muda mrefu wa Museveni aliripotiwa kukimbizwa katika kituo cha afya kilichopo Bugolobi Village Mall, jijini Kampala, kwa matibabu ya dharura, huku akisindikizwa na maafisa wa usalama kwa ulinzi mkali.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Buhweju, Francis Mwijukye, Besigye aliwasilishwa katika kituo hicho kilichopo ghorofa ya tatu akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu.

Maafisa wa usalama waliripotiwa kuzingira eneo hilo na kuweka vizuizi vinavyodhibiti harakati za watu ndani na nje ya kliniki hiyo, inayojulikana kama The Clinic.

Vyombo vya habari vya Uganda vinasema hata hivyo, uongozi wa The Clinic ulikataa kutoa maelezo kuhusu hali ya Besigye, ukisisitiza kuwa taarifa za wagonjwa ni za siri.

"Hii ni taasisi ya afya na tunafuata taratibu za usiri. Samahani, hatuwezi kutoa taarifa yoyote," alisema mfanyakazi mmoja wa kliniki hiyo alipoulizwa na wanahabari.

Naibu Meya wa Kampala, Doreen Nyanjura, ambaye ni mshirika wa karibu wa Besigye, alithibitisha kuwa mwanasiasa huyo anapata matibabu, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu hali yake.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved