logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Yoweri Museveni avunja kimya kuhusu kuzuiliwa na kuzorota kwa afya ya Kizza Besigye

Rais Museveni alidai kuwa udhaifu wa Besigye unahusiana zaidi na mgomo wake wa kula.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri18 February 2025 - 14:32

Muhtasari


  • Museveni ameweka wazi msimamo wake kuhusu kuzuiliwa kwa Besigye, akisisitiza kuwa kesi yake inapaswa kusikilizwa haraka ili ukweli ujulikane.
  • Kuhusu kucheleweshwa kwa kesi, alieleza kuwa Mahakama za Kijeshi ziliona dosari katika ushahidi na kuamuru kesi ihamishiwe Mahakama za Kiraia.

Yoweri Museveni na Kizza Besigye

 Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ameweka wazi msimamo wake kuhusu kuzuiliwa kwa aliyekuwa mpinzani wake wa muda mrefu, Dkt. Kizza Besigye, akisisitiza kuwa kesi yake inapaswa kusikilizwa haraka ili ukweli ujulikane.

Katika taarifa aliyotoa kwa umma, Museveni alieleza kuwa Besigye ameshikiliwa kwa tuhuma nzito zinazohusiana na usalama wa taifa.

Alisema badala ya wananchi kuhoji kwa nini Besigye amezuiliwa kwa muda mrefu, wanapaswa kuzingatia sababu ya kukamatwa kwake na umuhimu wa kusikilizwa kwa kesi hiyo haraka.

"Ikiwa unataka nchi tulivu, swali sahihi linapaswa kuwa: ‘Kwa nini Dkt. Besigye amekamatwa?’ Jawabu sahihi ni kuwa na kesi ya haraka ili ukweli uweze kufahamika. Vinginevyo, tunahatarisha usalama wa nchi, jambo ambalo ni hatari sana," alisema Museveni.

Kizza Besigye, ambaye amekuwa mpinzani wa muda mrefu wa Museveni tangu miaka ya 2000, amekamatwa mara kadhaa kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo uchochezi na kuandaa maandamano dhidi ya serikali.

Mwaka 2005, alikamatwa kwa tuhuma za uhaini na ubakaji, ingawa baadaye aliachiliwa kwa dhamana. Katika miaka ya hivi majuzi, amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Museveni, akipinga kile anachokiita udikteta na ukandamizaji wa haki za raia.

Museveni amekosoa wale wanaotaka Besigye aachiliwe kwa msamaha au dhamana, akisema kuwa mtazamo wa serikali yake ni kuhakikisha uwajibikaji kwa wote wanaovuruga usalama wa nchi.

Kuhusu kucheleweshwa kwa kesi ya Besigye, Museveni alieleza kuwa Mahakama za Kijeshi ziliona dosari katika ushahidi na kuamuru kesi ihamishiwe Mahakama za Kiraia. Alisema serikali na wabunge wanashughulikia marekebisho ya kisheria ili kuziba mianya hiyo na kuharakisha kesi za aina hii siku za usoni.

"Mahakama za Kijeshi zilikuwa tayari kwa kesi hiyo, lakini zilibaini baadhi ya mapungufu na kuamuru kesi ihamishiwe Mahakama za Kiraia. Hili ndilo limesababisha kucheleweshwa kwa mchakato," alifafanua Museveni.

Kuhusu hali ya afya ya Besigye, Museveni alisema kuna hospitali ya serikali ndani ya gereza, na kwamba madaktari wake binafsi wamekuwa wakimtembelea na hata kumpeleka kwenye kliniki binafsi kwa matibabu. Aliongeza kuwa iwapo kutahitajika matibabu zaidi, serikali iko tayari kutoa huduma hiyo.

Hata hivyo, Museveni alidai kuwa udhaifu wa Besigye unahusiana zaidi na mgomo wake wa kula, ambao alitaja kama jaribio la kushinikiza mahakama kuwa na huruma badala ya kusubiri kesi kusikilizwa.

"Kama mtu hana hatia, kwa nini hapiganii kesi ya haraka kuthibitisha hilo, badala ya mgomo wa kula ili kupata huruma ya kupewa dhamana?" alihoji Museveni.

Besigye aliripotiwa kuanza mgomo wa kula akiwa gerezani kama njia ya kupinga kizuizini chake.

Picha zake zilisambaa kwenye vyombo vya habari zikimuonyesha akiwa dhaifu, hali iliyozua mjadala mkubwa kuhusu afya yake. Hata hivyo, serikali inasisitiza kuwa hatua yake ni mbinu ya kisiasa ya kujipatia huruma ya umma.

Museveni alihitimisha kwa kusema kuwa kesi ya Besigye inapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria, na kwamba serikali haitaruhusu upotoshaji wa ukweli kwa manufaa ya kisiasa.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved