
Mahakama kuu nchini Uganda imewaamuru wakuu wa gereza wamrudishe gerezani kiongozi wa upinzani Dk. Kizza Besigye ambaye pia ni mgonjwa licha ya afya yake kuendelea kudhoofika.
Familia yake na mawakili wanaogopa kwamba kuendelea kuzuiliwa kwa mwanasiasa huyo mashuhuri ambaye yuko kwenye mgomo wa kususia chakula tangu wiki iliyopita kuhatarisha afya yake.
Akiongea baada ya kikao cha mahakama Winnie Byanyima, mke wa Dk. Kizza Besigye alisema amesikitishwa na maagizo ya mahakama.
"Nilikuja hapa nikitarajia kuondoka na Dk. Kizza Besigye kwenda naye nyumbani leo, nimeumia lakini sijashtuka. Besigye ni mateka, alitekwa nyara ”. Aliwaambia waandishi wa habari.
Besigye na mshitakiwa mwenzake Hajji Obeid Lutale walikuwa wamefika mahakamani katika mji mkuu Kampala kwa ajili ya kusikilizwa kwa ombi lililoletwa na mawakili wake wakitaka kuachiliwa kwake.
Hata hivyo, iliamuliwa kwamba Besigye ni mgonjwa na hakuweza kuendelea na kikao hicho. Aliamuru arudishwe gerezani ambapo ameshikiliwa kwa karibu miezi nne.
Besigye, daktari wa kibinafsi wa zamani wa Rais Yoweri Museveni, alikamatwa katika mazingira tata mnamo mwezi Novemba mwaka jana jijini Nairobi pamoja na msaidizi wake wa kisiasa, Obeid Lutale.
Wawili hao baadaye walifikishwa katika mahakama ya kijeshi huko Kampala, ambapo walishtakiwa kwa kumiliki silaha kinyume na sheria – madai ambayo wamekanusha.
Katika uamuzi wa kihistoria mwezi uliopita, Mahakama ya Juu Zaidi nchini Uganda ilitangaza kuwa ni kinyume na katiba kwa mahakama za kijeshi kusikiliza kesi za kiraia, na kuamuru kesi hiyo ihamishwe hadi katika mahakama za kiraia.
Uamuzi huo ulimkasirisha Rais Museveni, ambaye alisema ni "uamuzi mbaya" na kuapa kuupinga.
Katika ujumbe mrefu kwenye mtandao wa X, Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miongo minne alishutumu Mahakamana ya Juu Zaidi juu kwa 'kuchelewesha kesi ya Besigye, kufuatia uamuzi wake.
Wakati huo huo, wanasiasa wa upinzaji wakiongozwa na nyota wa zamani wa pop- Robert Kyagulanyi al maarufu Bobi Wine wanatarajiwa kufanya kikao cha pamoja cha maombi kwa ajili ya Besigye na wafungwa wengine wa kisiasa.
Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, viongozi wa upinzaji Jumatatu jioni, walitoa makataa ya saa 48 kwa serikali kumwachilia mwanasiasa mwenzi wao Kizza Besigye na wafungwa wote wa kisiasa.