
TIANJIN, CHINA, Septemba 1, 2025 – Rais wa China Xi Jinping
siku ya Jumatatu alitoa wito kwa wanachama wa Shirika la Ushirikiano wa
Shanghai (SCO) kuendelea mbele kwa hatua thabiti kwa ajili ya mustakabali bora
wakati shirika hilo likiendesha mkutano wake mkubwa zaidi katika jiji la
bandari la Tianjin nchini China.
Akihutubia Mkutano wa 25 wa Baraza la Wakuu wa
Nchi za SCO, Xi alitoa wito kwa wanachama kuendeleza “Roho ya Shanghai” katika
dunia yenye changamoto na mabadiliko, na kutumia vyema zaidi uwezo wa shirika
hilo.
Mafanikio Ya Kihistoria
SCO ilianzishwa mjini Shanghai mnamo Juni 2001
na imepanuka kutoka wanachama waanzilishi sita hadi kuwa shirika kubwa zaidi la
kikanda duniani, likihusisha zaidi ya maeneo 50 ya ushirikiano na pato la
kiuchumi la takriban dola trilioni 30 za Marekani.
“Ushawishi wake wa kimataifa na mvuto wake
unaongezeka kila siku,” Xi alisema, akitaja “mafanikio ya kihistoria na ya
msingi” katika maendeleo na ushirikiano wa SCO.
Alisema shirika hilo ndilo la kwanza kuanzisha
utaratibu wa kuaminiana kijeshi katika maeneo ya mipaka na kuzindua ushirikiano
wa Ukanda na Njia (Belt and Road). “Sisi ndio wa kwanza kukamilisha mkataba wa
ujirani mwema wa muda mrefu, urafiki na ushirikiano, tukitangaza dhamira yetu
ya kudumisha urafiki wa kudumu na kuepuka uhasama,” alisema.
Wanachama wa SCO pia walikuwa wa kwanza
kupendekeza maono ya utawala wa dunia kwa mashauriano ya kina, mchango wa
pamoja na manufaa ya pamoja, kama njia ya kutekeleza uhalisia wa uwingi wa
pande.
“Tunapaswa kuunga mkono dunia yenye nguvu
nyingi iliyo sawa na yenye mpangilio, pamoja na uliberali wa uchumi wa dunia
unaojumuisha wote na wenye manufaa kwa wote, na kufanya mfumo wa utawala wa
dunia uwe wa haki na usawa zaidi,” aliongeza.
Hatua Za Kiutendaji Zaidi
Xi alitoa wito kwa wanachama wa SCO kubaki wa
kweli kwa dhamira ya kuanzisha shirika hilo, na kuendeleza ukuaji wake endelevu
kwa azma kubwa na hatua za kivitendo zaidi.
Alisema wanachama wa SCO wanapaswa kutafuta misingi ya pamoja huku wakipuuza tofauti, kufuata manufaa ya pamoja, kushirikiana kwa uwazi na ujumuishi, kushikilia haki na usawa, na kujitahidi kwa matokeo halisi yenye ufanisi mkubwa.

“Wanachama wa SCO wote ni marafiki na
washirika,” alisema, akiwataka waheshimiane tofauti zao, kudumisha mawasiliano
ya kimkakati, kujenga makubaliano, na kuimarisha mshikamano na ushirikiano.
Xi alisema wanachama wanapaswa kutumia nguvu
za masoko yao makubwa na ukamilishaji wa kiuchumi, na kuboresha urahisishaji wa
biashara na uwekezaji.
Alitarajia ushirikiano kuimarishwa katika
nyanja kama vile nishati, miundombinu, viwanda vya kijani, uchumi wa
kidijitali, uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia, pamoja na akili bandia. Pia
alihimiza kuanzishwa haraka kwa benki ya maendeleo ya SCO.
Ili kuhakikisha maendeleo bora ya SCO kwa
hatua halisi, Xi alitangaza kuwa China itatoa msaada wa yuan bilioni 2
(takribani dola milioni 281 za Marekani) kwa wanachama wengine wa SCO ndani ya
mwaka huu, na kutoa mkopo wa ziada wa yuan bilioni 10 kwa benki wanachama wa
Muungano wa Mabenki wa SCO katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Zaidi ya hayo, China inapanga kutekeleza
miradi 100 ya kijamii midogo lakini yenye manufaa katika nchi wanachama wenye
uhitaji huo. Katika miaka mitano ijayo, China itaanzisha Warsha 10 za Luban
katika nchi hizo na kutoa nafasi 10,000 za mafunzo ya rasilimali watu.
Hisa ya uwekezaji wa China katika nchi
wanachama wa SCO imevuka dola bilioni 84 za Marekani, huku biashara yake ya
kila mwaka ya pande mbili na wanachama hao ikizidi dola bilioni 500 za
Marekani.
“China kila mara inalinganisha maendeleo yake na ya SCO na matakwa ya watu wa nchi wanachama kwa maisha bora,” Xi alisema.

Mkutano Mwenye Matokeo
Mkutano wa Jumatatu ulihusisha kutiwa saini na
kupitishwa kwa nyaraka kadhaa muhimu, ikiwemo Azimio la Tianjin na mkakati wa
maendeleo wa shirika hilo kwa kipindi cha 2026-2035, unaoonyesha dira ya SCO
kwa muongo ujao.
Viongozi wa nchi wanachama wa SCO
walikubaliana kukubali Laos kama mshirika wa mazungumzo wa shirika hilo, na
kuamua kuwa Kyrgyzstan itachukua urais wa zamu wa SCO kwa mwaka 2025-2026.
Matokeo ya mkutano huo pia ni pamoja na
taarifa ya kuunga mkono mfumo wa biashara wa pande nyingi, taarifa kuhusu
kumbukumbu ya miaka 80 ya ushindi wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kuanzishwa
kwa Umoja wa Mataifa, pamoja na nyaraka 24 za matokeo juu ya kuimarisha ushirikiano
katika nyanja kama vile usalama, uchumi na uhusiano wa kijamii, pamoja na
ujenzi wa shirika.
Vituo vipya vinne vya SCO vilizinduliwa kwa
ajili ya kukabiliana na vitisho na changamoto za usalama, kushughulikia uhalifu
uliopangwa wa kimataifa, kuboresha usalama wa taarifa, na kuimarisha
ushirikiano wa kupambana na dawa za kulevya.
Viongozi wa nchi wanachama wa SCO, pamoja na
Katibu Mkuu wa SCO Nurlan Yermekbayev, na Mkurugenzi wa Kamati ya Utendaji ya
Muundo wa Kikanda wa SCO wa Kupambana na Ugaidi Ularbek Sharsheev, walitoa
hotuba katika mkutano huo.
Walisema kuwa katika uso wa dunia yenye misukosuko, nchi wanachama wa SCO zinapaswa kuongeza uratibu wa kimkakati, kukataa upendeleo wa upande mmoja, ubabe na ulinzi wa kibiashara, kuboresha mfumo wa utawala wa dunia, na kushikilia haki na usawa wa kimataifa.