Jackton Odhiambo, mshukiwa mkuu katika mauaji ya mwanaharakati wa LGBTQ Edwin Kiprotich Kiptoo maarufu kama Chilloba anatarajia kusikiliza hukumu dhidi yake mnamo Disemba 16, 2024 baada ya mahakama kuu ya Eldoret kumpata na hatia katika kesi iliyosikilizwa Jumatano Disemba 4.
Hukumu kwa Jackton inajiri takribani miaka miwili tangu kuripotiwa kwa kuawa kwa ‘Chiloba’ katika eneo la Kimumu, jijini Eldoret mnamo Disemba 31, 2022.
Akitoa uamuzi wa kesi hiyo, jaji Reuben Nyakundi wa mahakama kuu ya Eldoret alisema kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha ulioonyesha kuwa mshukiwa alitekeleza mauaji hayo. Kwa mujibu wa jaji huyo, ushahidi uliowasilishwa kortini humo na mashahidi pamoja na chembechembe za msimbo jeni ziliashiria kuhusika kwa Jackton katika mauaji ya ‘Chiloba’.
“Korti hii katika uamuzi wake, mtuhumiwa Jackson Odhiambo maarufu kama Lisa ana hatia ya mauaji kinyume na kifungu cha 203 ya kanuni za adhabu.” Alisema jaji Nyakundi.
Vile vile, ushahidi uliowasilishwa mahakamani na mashahidi ulionyesha kuwa Jackton Odhiambo ndiye mtu wa mwisho aliyeoonekana katika sehemu moja ya burudani katika jiji la Eldoret usiku wa tukio hilo.
Awali Jackton alikuwa ameshtakiwa pamoja na washukiwa wengine wanne ambao waliwachiliwa huru baada ya mahakama kuwapata bila hatia.
Mwili wa ‘Chiloba’ ulipatikana ndani ya sanduku kubwa la
chuma katika eneo la Kipkenyo zaidi ya kilomita nane kutoka eneo lililoshukiwa
kuwa la uhalifu.