
MWANAJESHI mmoja wa kike aliripotiwa kubakwa hospitalini alikokuwa amelazwa baada ya kupatwa na hitilafu ya kiafya akiwa mazoezini.
Tukio hili la kuajabisha na kusikitisha lilitokea nchini
Zambia ambapo daktari alimbaka mwanajeshi huyo aliyepelekwa kwa huduma ya
matibabu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Maambo Hamaundu
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana na mhusika yuko chini ya ulinzi.
Wizara ya Ulinzi nchini humo ililaani yaliyojiri na
kuwahakikishia umma kwamba hakuna mtu atakayelindwa katika uchunguzi huo.
"Menejimenti ya
Kituo cha Matibabu cha Maina Soko inashirikiana na uchunguzi wa Polisi ili haki
itendeke," alisema mkuu wa wizara, Hamaundu.
Kulingana na vyanzo vya uhakika kutoka kwa Kituo cha Matibabu
cha Maina Soko, mgonjwa huyo ni mwajiriwa wa Jeshi la Zambia ambaye aliugua
wakati wa mafunzo na alipelekwa hospitali kwa matibabu.
Matukio ya madaktari kuwabaka wagonjwa hospitalini si mageni
kwani humu nchini Kenya wiki kadhaa zilizopita, daktari mmoja katika kaunti ya
Mombasa alituhumiwa kwa kumtendea unyama mgonjwa wa kike.
Daktari huyo alifikishwa mbele ya hakimu mkuu Alex Ithuku
katika mahakama kuu ya Mombasa mapema Februari ambapo alishtakiwa kwa kosa moja
la ubakaji.
Alishtakiwa kwa kumbaka mgonjwa saa kumi na moja asubuhi
tarehe 31 Januari 2025 katika hospitali ya Pandya, ambaye alikuwa akitafuta
huduma ya kusafisha damu katika kituo hicho.
Hata hivyo alikanusha shtaka hilo na kuachiliwa kwa dhamana
na mdhamini wa kiasi sawa na hicho.
Shirika la kutetea haki za wanawake FIDA lililaani kisa
hicho, likisema kuwa mwanamke huyo alibakwa hapo awali na mshukiwa huyo, na
kutaka watu wengine zaidi wakamatwe ambao waliwatuhumu kwa kukwamisha mwenendo
wa haki.
Shirika hilo lilitoa wito kwa DCI kufanya uchunguzi dhidi ya
unyama huo na kutaka hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mtendaji kama
njia moja ya kuzima kabisa visa vya dhuluma dhidi ya wanawake.