logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kutoka Argentina hadi Vatican - Mfahamu zaidi marehemu Papa Francis

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, alifariki dunia mnamo Aprili 21, Jumatatu ya Pasaka.

image
na Samuel Mainajournalist

Makala22 April 2025 - 07:52

Muhtasari


  • Papa Francis alifariki siku ya Jumatatu asubuhi katika makaazi yake ya Casa Santa Marta, ndani ya mji wa Vatican.
  • Papa Francis, ambaye jina lake halisi lilikuwa Jorge Mario Bergoglio, alichaguliwa kuwa Papa mnamo Machi 13, 2013.

Pope Francis/ FILE

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, alifariki dunia siku ya jana, Jumatatu ya Pasaka, Aprili 21, 2025, akiwa na umri wa miaka 88.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Vatican kupitia ukurasa wao wa X, Papa Francis alifariki saa moja na dakika thelathini na tano asubuhi katika makaazi yake ya Casa Santa Marta, ndani ya mji wa Vatican.

Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Vatican, ndiye aliyetangaza rasmi kifo hicho kwa kusema:

“Saa 1:35 asubuhi ya leo, Askofu wa Roma, Francis, amerudi nyumbani kwa Baba. Maisha yake yote aliyaweka wakfu kwa kumtumikia Bwana na Kanisa lake. Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa uaminifu, ujasiri, na upendo wa kweli – hasa kwa maskini na waliotengwa.”

Aliendelea kwa kusema:“Kwa shukrani kubwa kwa mfano wake kama mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo, tunaikabidhi roho ya Papa Francis kwa upendo wa Mungu usio na mwisho.”

Papa Francis, ambaye jina lake halisi lilikuwa Jorge Mario Bergoglio, alichaguliwa kuwa Papa mnamo Machi 13, 2013, na alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini, na wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,200.

Taarifa ya Vatican pia ilieleza kuwa Papa Francis alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli mjini Roma tangu Ijumaa ya Februari 14, 2025, kufuatia matatizo ya kupumua yaliyosababishwa na bronkaitisi. Tarehe 18 Februari, madaktari walibaini kuwa alikuwa na nimonia ya mapafu yote mawili (bilateral pneumonia), hali iliyozidi kudhoofisha afya yake.

Baada ya kukaa hospitalini kwa siku 38, aliruhusiwa kurejea nyumbani Vatican mnamo Machi 23 ili kuendelea na matibabu akiwa chini ya uangalizi wa karibu. Hata hivyo, hali yake iliendelea kuzorota hadi alipoaga dunia jana asubuhi.

Kifo chake kimewaacha waumini wa Kanisa Katoliki na jumuiya ya kimataifa wakiwa na huzuni kubwa, wakikumbuka uongozi wake wa upole, huruma, na msimamo wake wa haki kwa wanyonge, mazingira, na mshikamano wa binadamu.

Vatican inatarajiwa kutangaza ratiba ya mazishi na mchakato wa kumchagua Papa mpya katika siku chache zijazo.

Huku ulimwengu ukiendelea kumuomboleza kiongozi huyo wa Katoliki, tumekuandalia maelezo Zaidi kumhusu marehemu;

>Mzaliwa wa Buenos Aires, Argentina.

>Mwanawe Mario na Regina Sivori- Wahamiaji kutoka Italia.

>Ana umri wa miaka 88.

>Alisoma kozi ya Ufundi wa Kemikali.

>Shahada ya Falsafa kutoka Chuo cha San Jose (Argentina), 1963

>Shahada ya Theolojia kutoka Chuo Cha San Jose, 1970

>Alitawazwa kama padri, Dec 1969.

>Aliteuliwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, Feb 1998.

>Alifanywa Kardinali na Papa John Paul II mnamo 2001.

>Alichaguliwa kuwa Papa, Machi 2013.

>Papa wa Kwanza kutoka Amerika.

>Ilichapisha kitabu cha kumbukumbu "Hope", Jan 2025

>Sehemu ya mapafu yake ilitolewa wakati wa ujana wake.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved