“Mimi ni baba mwenye fahari!” Raila awapongeza vijana waliojitokeza kwa wingi kuandamana

Alichapisha video ya kijana mmoja wa kike akiandamana huku akijirekodi na kusema kwamba alijihisi baba mwenye fahari kuona vijana wadogo wameamua kujitokeza kwenye barabara kupigania haki zao.

Muhtasari

• Hata hivyo, shinikizo la vijana dhidi ya serikali lilionekana kuzaa matunda kidogo kwani baadhi ya vipengele tata kwenye mswada huo viliondolewa.

RAILA ODINGA
RAILA ODINGA
Image: FACEBOOK

Kinara wa muungano wa upinzani Raila Odinga ameonyesha fahari yake kwa mamia ya vijana waliojitokeza siku ya Jumanne katikati mwa jiji la Nairobi kuandamana dhidi ya mswada wa kifedha wa 2024.

Jumanne, jiji la Nairobi lilishuhudia shughuli nyingi za kiuchumi zikisitishwa kwa takribani mchana kutwa huku vijana wakijumuika kwa wingi kukimbizana na polisi na vitoza machozi kwa kile walidai ni mswada dhalimu wa kifedha.

Odinga kupitia ukurasa wake wa X, alichapisha video ya kijana mmoja wa kike akiandamana huku akijirekodi na kusema kwamba alijihisi baba mwenye fahari kuona vijana wadogo wameamua kujitokeza kwenye barabara kupigania haki zao.

“Ninajihisi kuwa baba mwenye fahari leo!  Hongera sana kwa mwanadada na wale wote waliosimama kishujaa kutetea haki zao!” Odinga alisema.

Katika video hiyo, binti huyo alijirekodi akituma ujumbe kwa Odinga akimtaka asijitokeze kweney maandamano kwao vijana wenyewe waliamua kujitokeza kwa niaba yake ili kuishinikiza serikali kutupilia mbali mswada huo ambao wanahisi utawafinya Zaidi kiuchumi.

Ifahamike kwamba shughuli za maandamano dhidi ya serikali katika kipindi cha miaka mingi sasa zimekuwa zikihusishwa na kinara huyo wa ODM ambaye kwa mara nyingi anajipata kwenye mrengo wa upinzani.

Hata hivyo, shinikizo la vijana dhidi ya serikali lilionekana kuzaa matunda kidogo kwani baadhi ya vipengele tata kwenye mswada huo viliondolewa.

Mwenyekiti wa kamati ya mswada huo, ambaye ni mbunge wa Molo Kimani Kuria alitangaza kwamba wamewasikiliza Wakenya na kuamua kuondoa baadhi ya vipengele ikiwemo ile ya ushuru wa VAT kwa mkate, ushuru kwa umiliki wa magari na pia kufichua kwamba walikuwa wanatathmini kuondoa ushuru kwa mafuta ya kula na usafirishaji wa sukari.

Mswada huo unatarajiwa kuanza kujadiliwa katika bunge la kitaifa leo Jumatano asubuhi.