Mwanapatholojia mkuu
wa serikali Dkt Johansen Oduor amethibitisha kwamba mwanaharakati wa Molo
aliyeuawa ,Richard Otieno, alifariki kutokana na majeraha ya kichwa
yaliyosababishwa na kifaa chenye ncha kali.
Otieno aliuawa nje ya nyumba yake katika mji wa Elburgon, kaunti ya Nakuru, usiku wa Jumamosi, Januari 18, na watu wasiojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa, Oduor alisema kuwa silaha iliyotumiwa kumsababishia Otieno majeraha kichwani inaweza kuwa shoka au panga.
"Kulikuwa na majeraha kadhaa mabaya, ikiwa ni pamoja na majeraha mengi ya kukatwa sehemu ya nyuma ya kichwa, ambayo yalisababisha kuvunjika kwa fuvu na kuvuja damu nyingi kwenye ubongo," Oduor alisema.
Mwanapatholojia huyo alisema hayo baada ya kufanya uchunguzi wa maiti siku ya Ijumaa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kericho County Level Five.
"Pia kulikuwa na majeraha ya kukatwa sehemu ya mbele ya fuvu la kichwa, ingawa hayakusababisha kuvunjika," aliongeza.
Otieno ambaye alikuwa mkosoaji mkali wa serikali, alijulikana kama 'Rais wa Molo'.
Aliuawa kwa kukatwakatwa siku mbili baada ya kulalamika kuwa alikuwa akipokea vitisho na kuandamwa na watu watatu wasiojulikana.
Mwanaharakati huyo aliyezungumza waziwazi alipatikana ameuliwa karibu na nyumba yake, mita chache kutoka kituo cha polisi cha Elburgon.
Oduor alisema walikusanya sampuli kutoka kwa mwili wake kwa uchunguzi zaidi.
"Watu wawili wanapohusika katika ugomvi mkali, mara nyingi hubadilishana nyenzo za DNA. Sampuli zitakazokusanywa zitasaidia kuwatambua wahusika. Pia tulikusanya sampuli za kucha kwa ajili ya uchunguzi wa DNA ili kubaini iwapo marehemu alikuwa na kitu chochote kabla ya kukutana na washambuliaji wake," alieleza.
Maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya uchunguzi wa Mauaji ya DCI wanashughulikia kesi hiyo ili kubaini waliohusika na mauaji hayo ya kutatanisha.
Familia ya Otieno, ambao walikuwa miongoni mwa waliokuwepo wakati wa uchunguzi wa maiti, walidai haki kwa mpendwa wao.
Wengine waliokuwepo wakati wa zoezi hilo ni mwanasheria wa familia na maafisa kutoka Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR).