
Mwili wa Martin Mwau, mhasiriwa wa pili kati ya wanaume watatu waliotoweka nyara eneo la Mlolongo mwezi Desemba mwaka jana, umepatikana katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City.
Kupatikana kwa mwili wa Martin kulijiri muda mchache baada ya mwili wa mhasiriwa wa pili Justus Mutumwa kutambuliwa katika hifadhi hiyo ya maiti.
Mutumwa alikuwa ametoweka mnamo Desemba 16, 2024, akiwa pamoja na Mwau na Karani Muema. Kwa zaidi ya mwezi mmoja, familia zao zilikuwa zikitafuta majibu kuhusu kutoweka kwao.
Kulingana na familia ya Mutumwa, mwili wake ulichukuliwa kutoka eneo la Ruai na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti mnamo Desemba 18, siku mbili tu baada ya kutoweka.
Haijulikani ni wapi mwili wa Mwau ulipatikana kabla ya kupelekwa katika kituo hicho.
Kupatikana kwa mwili wa Mwau kunazidisha wasiwasi juu ya hali ya kutoweka kwa watatu hao na vifo vya wawili huku mwingine akiwa bado hajulikani aliko.
Baada ya kupuuza wito mwingi wa mahakama, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohammed Amin hatimaye walifikishwa mahakamani siku ya Alhamisi, ambapo walikanusha kufahamu waliko watatu hao.
Amin alisema kuwa suala hilo bado linachunguzwa.
Huku watu wawili kati ya watatu waliotoweka wakithibitishwa kufariki, shinikizo linaongezeka kwa taasisi husika kutoa majibu na kuhakikisha haki kwa waathiriwa na familia zao.