
Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi kwa mara nyingine ameikosoa serikali kuhusiana na visa vya utekaji nyara na mauaji ya kiholela.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha City, ambapo miili ya vijana wawili kati ya wanne waliotekwa nyara huko Mlolongo ilipatikana, Muturi alielezea kughadhabishwa na kuendelea kutoweka na mauaji ya vijana wa Kenya.
"Haya ni mauaji mabaya zaidi. Ni haki tu kwamba, kwa wakati huu, nchi itaweka kando shughuli zingine zozote kujadili suala hili la utekaji nyara na mauaji ya kiholela,” Muturi alisema.
Muturi ambaye awali alishtumu polisi kufuatia kutekwa nyara kwa mwanawe mwaka jana alisema hakuna vile serikali itajigamba kustawisha uchumi wa nchi huku vijana wa taifa wanatekwa na kuuawa.
“Si sawa kwamba wazazi kama hawa wanaweza kwenda kwa zaidi ya siku 40 kutafuta wapendwa wao na sisi tunakaa mahali tukijidai kujadili uchumi. Uchumi kwa nani? Ikiwa tunaua na kuwateka vijana, basi tunajenga uchumi kwa ajili ya nani?” Waziri aliuliza.
Muturi alikashifu kile alichotaja kuwa kuhalalishwa kwa mauaji ya kiholela, akisema serikali ina jukumu la kulinda raia wake badala ya kusimamia vifo vyao.
Alisema kwamba wakati wa kampeni, Rais Ruto aliapa kukomesha utekaji nyara, lakini matukio haya bado yanaendelea.
“Rais, naomba sasa utoe agizo la kukomesha vitendo hivi vya utekaji nyara na uanzishe uchunguzi kuchunguza jinsi mambo haya yamekuwa yakifanyika. Haya ni maisha changa sana ambayo yamechukuliwa. Wazazi wao wamekuwa wakiteseka,” alisema.
Alipendekeza kuundwa kwa tume ya uchunguzi itakayojumuisha wawakilishi kutoka Chama cha Wanasheria wa Kenya, makundi ya kidini, na mashirika ya kiraia kama vile Amnesty International Kenya na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya ili kubaini ukweli.
Waziri huyo pia alitilia shaka jitihada za Kenya za kidiplomasia akihoji vile Kenya itatatua mgogoro katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ilhali imeshindwa kushughulikia mauaji ndani ya mipaka yake.
“Kwa nini tunaruhusu vijana kutekwa nyara na baadaye kupatikana wameuawa? Sisi ni nchi gani na tunajifanya kuwa tunasuluhisha maswala huko DRC,” Muturi alisema.
Matamshi ya Muturi yanajiri baada ya miili ya Martin Mwau na Justus Mutumwa ambao walikuwa miongoni mwa vijana wanne waliotoweka Mlolongo Desemba mwaka jana kupatikana katika hifadhi ya maiti ya City mjini Nairobi.