
Naibu Rais aliyetimuliwa, Rigathi Gachagua, amesema hawezi kufuta uwezekano wa kushirikiana na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, kabla ya uchaguzi wa 2027.
Akizungumza kwenye mahojiano na KTN siku ya Jumatatu, Gachagua alieleza kuwa yuko tayari kufanya kazi na kiongozi yeyote anayenuia mema kwa mustakabali wa Kenya.
"Niko wazi kushirikiana na yeyote ambaye ana nia njema kwa nchi hii. Nataka kuwaambia wafuasi wa Raila kutoka Nyanza wasipigane na watu wa Mlima Kenya kwa sababu sisi si maadui wao," alisema.
Gachagua alifafanua kuwa watu wa eneo la Mlima Kenya hawana tatizo na Raila Odinga, bali changamoto yao kuu ni utawala wa Kenya Kwanza.
"Hatuna pingamizi lolote la kushirikiana na Raila. Tayari tunafanya kazi na Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, na viongozi wengine wenye mawazo yanayofanana nasi," alisisitiza.
Aidha, Gachagua alikosoa dhana kwamba jamii ya Mlima Kenya inampinga Raila, akisema kuwa ni makosa kuhukumu jamii nzima kwa matendo ya watu wachache waliodhihirisha furaha baada ya Raila kushindwa katika kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AUC).
"Baadhi ya watu wanawalaumu watu wa Mlima Kenya kwa kushindwa kwa Raila kwa sababu tu wanawake wachache huko Kirinyaga walisherehekea kushindwa kwake," aliongeza.
Naibu rais huyo wa zamani alisema kuwa baada ya kufanya mashauriano na wananchi kupitia mikutano 450 katika miezi minne iliyopita, amegundua kuwa kuna haja ya kutafuta marafiki wapya wa kisiasa.
Kwa upande mwingine, Gachagua alibainisha kuwa hana tatizo na Raila licha ya kwamba wabunge wa ODM walipigia kura hoja ya kumwondoa madarakani.
"Si Raila aliyepanga hoja ya kuniondoa madarakani," alieleza.
Matamshi haya yanaashiria mwelekeo mpya wa kisiasa wa Gachagua, huku siasa za uchaguzi wa 2027 zikiendelea kuchukua sura mpya.