
Kiongozi wa chama cha People’s Liberation Party (PLP), Martha Karua, amesema kuwa licha ya kuwa na tofauti za kisiasa, yeye anamchukulia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kama ndugu yake, sawa na Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Akizungumza katika mahojiano na Citizen TV Jumatano, Karua alieleza kuwa yeye na Gachagua wana nia moja ya kushirikiana kwa manufaa ya Wakenya, kwani wote wanatamani kuona mateso ya wananchi yakipungua.
“Rigathi Gachagua ni Mkenya, na ni ndugu yangu, kama vile Ruto na Raila walivyo ndugu zangu, japokuwa hatuko katika upande mmoja wa kisiasa,” alisema.
Alifafanua kuwa kwa sasa, yeye na Gachagua wanashirikiana kwa lengo la kupigania haki za wananchi na kupunguza mzigo mzito waliobeba.
“Kwa sasa, tunasimama pamoja na viongozi wengine wenye nia
njema ili kuhakikisha Wakenya wanapata afueni kutokana na hali ngumu
wanayopitia. Katika hili, sisi ni washirika,” aliongeza.
Karua pia alieleza kuwa muungano wa kisiasa kati yao ni jambo lisiloepukika, ingawa halitafanyika mara moja.
“Kuna uwezekano wa muungano. Huenda isiwe leo, lakini ni jambo litakalotokea. Kwa sasa, haiwezekani kupiga hatua kubwa kisiasa bila kushirikiana,” alisema.
Kauli yake inajiri baada ya mkutano wake na Gachagua katika nyumbani kwake ya kijijini wiki chache zilizopita, ambapo walifanya mazungumzo kuhusu hali ya nchi.
Baada ya mkutano huo, Gachagua alieleza kuwa amekubaliana na Karua kushirikiana na viongozi wengine ili kutafuta mwelekeo mzuri kwa taifa.
“Tumejadiliana kwa kina na tumeamua kushirikiana na Wakenya wanaotaka uongozi wenye maadili. Watu wengi wanatafuta viongozi wanaojali maslahi ya taifa, na tupo tayari kufanya kazi pamoja,” alisema Gachagua.
Aliongeza kuwa anamfurahia Karua kama mshirika mpya wa kisiasa, akisema kuwa uzoefu wake na uthabiti wake vitakuwa na mchango mkubwa, hasa katika ukanda wa Mlima Kenya.
“Tutapata mwongozo mzuri kutoka kwake. Tutashauriana naye mara kwa mara pamoja na viongozi wengine wenye maono mema kwa taifa ili kuleta mabadiliko,” alisema.
Karua pia alielezea imani yake kuwa ushirikiano wao utaleta nguvu mpya katika siasa za nchi.
“Siku ya leo ni mwanzo wa safari mpya. Tumekubaliana kushirikiana katika juhudi za kuunganisha na kulikomboa taifa letu. Tunakaribisha watu kutoka maeneo yote kushirikiana nasi katika mapambano ya kutetea haki za wananchi,” alisema.