logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Vatican yafichua hali ya Papa Francis baada ya kukumbwa na matatizo makali ya kupumua

Taarifa iliyotolewa Jumanne asubuhi pia ilieleza kuwa kiongozi huyo wa kidini anaendelea kupokea tiba maalum.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri04 March 2025 - 15:18

Muhtasari


  •  Papa Francis, aliweza kulala vizuri usiku wa Jumatatu na anaendelea kupumzika chini ya uangalizi wa madaktari,  Vatican imesema.
  • Kwa sasa, ameanza kutumia tena oksijeni ya mtiririko wa juu kupitia bomba la pua.

Pope Francis funeral is being rehearsed after warning he may not survive.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, aliweza kulala vizuri usiku wa Jumatatu na anaendelea kupumzika chini ya uangalizi wa madaktari, kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Vatican.

Taarifa hiyo iliyotolewa Jumanne asubuhi pia ilieleza kuwa kiongozi huyo wa kidini anaendelea kupokea tiba maalum ya mfumo wa kupumua na mwili kwa jumla.

"Papa alilala usiku kucha na sasa anaendelea kupumzika," ilisema Ofisi ya Habari ya Vatican Jumanne asubuhi.

Papa Francis, ambaye ana umri wa miaka 87, amelazwa katika Hospitali ya Gemelli, Roma tangu Februari 14 kutokana na nimonia ya mapafu yote mawili. Ingawa hali yake imekuwa changamano, madaktari wanasema kwa sasa inaonekana kuwa tulivu.

Kwa sasa, ameanza kutumia tena oksijeni ya mtiririko wa juu kupitia bomba la pua (nasal cannula), lakini hajawekewa mashine ya kupumulia moja kwa moja.

Asubuhi ya Jumanne, alitumia muda wake kupumzika na kusali huku akiendelea kupatiwa uangalizi wa karibu kutoka kwa madaktari wa Serikali ya Vatican na jopo la Hospitali ya Gemelli.

Jumatatu usiku, hali ya Papa ilizorota baada ya kupata matatizo mawili ya kupumua kwa ghafla. Vatican ilieleza kuwa hali hiyo ilisababishwa na mkusanyiko mkubwa wa kamasi kwenye mirija ya kupumulia, hali iliyopelekea kubana kwa bronchi (bronchospasm).

"Kulikuwa na vipindi viwili vya upungufu mkali wa hewa, vilivyosababishwa na mkusanyiko wa kamasi na matokeo yake yakawa bronchospasm," ilisema Vatican.

Madaktari walifanya bronchoscopy mara mbili kuondoa kamasi hiyo na kumsaidia kupumua vizuri. Baada ya matibabu hayo, alihitaji msaada wa kupumua kwa muda mfupi kwa kutumia mfumo wa upumuaji usiohusisha mashine kubwa.

Licha ya changamoto hizo, Vatican iliripoti kuwa wakati wote wa matibabu, "Baba Mtakatifu alibaki macho, mwenye fahamu timamu, na aliendelea kushirikiana vyema na madaktari wake."

Vipimo vya damu vilionesha kuwa hana maambukizi mapya ya mfumo wa hewa, kwani hakukuwa na ongezeko la seli zake nyeupe za damu. Hata hivyo, madaktari wameonya kuwa uwezekano wa matatizo zaidi ya upumuaji bado upo.

Kwa sasa, hali yake inaendelea kuwa ya tahadhari, huku waumini wa Kanisa Katoliki duniani kote wakiendelea kumuombea afya njema na ahueni ya haraka.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved