
Ofisi ya Habari ya Vatican imetoa taarifa mpya kuhusu hali ya
afya ya Papa Francis, ikithibitisha kuwa Baba Mtakatifu alipata usingizi mzuri
usiku wa kuamkia Jumatano, Machi 5, 2025, katika Hospitali ya Gemelli mjini
Rome.
Kwa mujibu wa Vatican, Papa Francis, mwenye umri wa miaka 87, anaendelea kupokea matibabu ya nimonia aliyogunduliwa nayo tangu Februari 14.
Usiku wa Jumanne, aliendelea kutumia mashine ya kusaidia kupumua isiyo ya upasuaji, kama sehemu ya matibabu yaliyoratibiwa na madaktari wake.
Taarifa ya Jumanne jioni ilieleza kuwa hali yake ya kliniki ilibaki thabiti siku nzima.
"Papa hakuwa na homa, alibaki macho, akiwa na fahamu timamu, na akishirikiana vyema na madaktari katika matibabu," ilisema Ofisi ya Habari ya Vatican.
Asubuhi ya Jumatano, Baba Mtakatifu alihamishiwa tiba ya oksijeni yenye mtiririko wa juu na kufanyiwa tiba ya mwili kwa ajili ya mfumo wa kupumua. Kulingana na taarifa mpya iliyotolewa leo,
"Papa alipumzika vyema usiku wa jana na aliweza kuamka muda mfupi baada ya saa mbili asubuhi,” ilisema Vatican.
Tangu alipoanza kupata matibabu, waumini wa Kanisa Katoliki na watu kutoka dini na mataifa mbalimbali wameonyesha mshikamano wao kupitia sala na ujumbe wa faraja kwa Baba Mtakatifu. Katika maeneo mengi duniani, ibada na maombi maalum yamefanyika kwa ajili ya afya yake.
Madaktari wa Vatican wanaendelea kufuatilia hali ya afya ya Papa Francis kwa karibu, huku akibaki hospitalini kwa uangalizi wa kitaalamu. Licha ya changamoto za awali, madaktari wamesisitiza kuwa hatua zinazoshuhudiwa sasa zinatoa matumaini ya kupona kwake.
Kwa sasa, ulimwengu unasubiri taarifa zaidi kutoka Vatican, huku waumini wakiendelea kumuombea Baba Mtakatifu afya njema na kurejea haraka kwenye majukumu yake rasmi.