logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Kwa nini Wafuala Chebukati aliishi zaidi ya miezi aliyotabiriwa - mkewe afichua

Chebukati, alipewa muda wa kuishi wa miezi sita baada ya kugunduliwa na saratani ya ubongo mwaka wa 2023.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri08 March 2025 - 15:10

Muhtasari


  • Chebukati aliendelea kuishi kwa takriban miaka miwili, jambo ambalo familia yake inasema lilichangiwa na upendo na msaada mkubwa aliopokea.
  • Kwa mujibu wa mkewe, watoto wao walikuwa chanzo kikuu cha nguvu kwake wakihakikisha wanamtembelea mara kwa mara na kumpa faraja. 

Wafula Chebukati

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, alipewa muda wa kuishi wa miezi sita baada ya kugunduliwa na saratani ya ubongo aina ya glioblastoma mwaka wa 2023.

Hata hivyo, aliendelea kuishi kwa takriban miaka miwili, jambo ambalo familia yake inasema lilichangiwa na upendo na msaada mkubwa aliopokea.

Akizungumza wakati wa mazishi ya mumewe katika kijiji cha Kiminini, Kaunti ya Trans Nzoia, mkewe Mary Chebukati alisema kuwa ingawa ugonjwa huo ulikuwa na makadirio mabaya, Chebukati alipata nguvu kutokana na uwepo wa familia, marafiki na viongozi waliomsimamia katika kipindi kigumu. 

"Ukitafuta kwenye mtandao kuhusu glioblastoma, utaona makadirio ni miezi minne hadi sita. Lakini mwenyekiti aliishi miezi 21, na hii ni kwa sababu ya msaada mkubwa alioupata," alisema Mary.

Kwa mujibu wa Mary, watoto wao Jonathan, Rachel na Emmanuel walikuwa chanzo kikuu cha nguvu kwa baba yao, wakihakikisha wanamtembelea mara kwa mara na kumpa faraja. 

"Watoto wangu hawa mnaowaona hapa ndio walikuwa nguvu ya mwenyekiti kuendelea kuishi muda mrefu," alieleza Mary huku akiwashukuru madaktari waliomhudumia mumewe.

Rachel Chebukati, binti yake, alikumbuka jinsi baba yao alivyopambana licha ya madaktari kusema kwamba alikuwa na miezi michache ya kuishi.

"Alipoambiwa ana muda wa miezi minne hadi sita tu, baba alisema ugonjwa huu haunishindi. Aliendelea kupokea matibabu, akafanyiwa upasuaji wa kwanza kwa msaada wa Mheshimiwa Rais, akarudi nyumbani na ungeweza kudhani hana tatizo lolote," alisema Rachel.

Mary pia alieleza jinsi madaktari walivyoshangazwa na jinsi mumewe alivyoendelea kuishi kwa muda mrefu zaidi ya matarajio yao.

"Madaktari walisema walishangazwa na uimara wake, lakini walituambia wazi kuwa sababu kubwa ilikuwa ni upendo na msaada aliopata kutoka nyumbani. Walisema hawajawahi kuona mgonjwa akisimamiwa kwa kiwango hicho," alifichua.

Katika hotuba yake, Mary alitoa shukrani kwa Rais William Ruto na viongozi wengine wa kisiasa na kidini kwa kuwa bega kwa bega na familia yao wakati wa mapambano ya Chebukati na ugonjwa huo.

Mazishi ya Chebukati yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wanasiasa, na marafiki wa familia, huku wakimsifu kama kiongozi aliyekuwa na maadili thabiti na mchango mkubwa kwa taifa.

 Glioblastoma ni nini?

Kwa mujibu wa madaktari, glioblastoma ni aina ya saratani ya ubongo inayojulikana kwa ukuaji wake wa haraka na uchokozi. Saratani hii huathiri zaidi watu wazima na mara nyingi huchukua muda mfupi kabla ya kuwa hatari. 

Kwa kawaida, wagonjwa wa glioblastoma hupewa muda wa kuishi wa miezi 4-6 baada ya kugunduliwa, lakini Chebukati aliweza kuishi kwa zaidi ya miezi 21, jambo ambalo Mary anasema lilitokana na msaada mkubwa wa familia na marafiki.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved