
Mvutano wa kisiasa kati ya Seneta wa Nyeri, Wahome Wamatinga, na aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, umechukua mkondo mpya baada ya Wamatinga sasa kumtaka Gachagua kuomba radhi hadharani ndani ya saa 48..
Hii ni kufuatia madai ya Gachagua kwamba Wamatinga alipokea hongo ya Ksh.10 milioni ili kupiga kura ya kumuondoa madarakani wakati wa kesi ya kumbandua naibu rais huyo wa zamani mwezi Oktoba 2024.
Katika hotuba yake mnamo Machi 2, 2025, katika kaunti ya Machakos, Gachagua alidai kuwa baadhi ya maseneta walihongwa ili kumuondoa madarakani kupitia kura ya Seneti. DP huyo wa zamani alimhusisha Wamatinga na madai ya kupokea hongo, jambo ambalo amelipinga vikali.
Kupitia wakili wake, Wycliffe Nyabuto, Wamatinga amemtaka Gachagua kuomba msamaha hadharani, akimtuhumu kwa kumchafulia jina na kuharibu sifa yake mbele ya umma.
"Mteja wangu hajawahi kupokea pesa yoyote kwa ajili ya kupiga kura yoyote dhidi ya yeyote. Madai haya ni ya uongo na yanalenga kumharibia jina kisiasa," ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Machi 7, 2025.
Seneta Wamatinga alieleza kuwa uamuzi wake wa kupiga kura katika Seneti ulitokana na ushahidi uliowasilishwa na wala haukuhusisha ushawishi wa kifedha. Alionya kuwa iwapo Gachagua hatatoa msamaha hadharani kufikia Machi 9, 2025, atachukua hatua za kisheria mara moja.
Tangu kuondolewa kwa Gachagua madarakani mnamo Oktoba 17, 2024, kwa tuhuma za ukiukaji wa katiba na uongozi mbaya, mvutano wa kisiasa kati yake na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya umeendelea kuongezeka.
Wamatinga, ambaye hapo awali alionekana kuwa mfuasi wa Gachagua, sasa ameonekana kuwa na misimamo tofauti naye, jambo ambalo limeibua mjadala mpana katika ulingo wa kisiasa.
Wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa hali hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa za Mlima Kenya, hasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Wengi wanaona kwamba mgawanyiko huu unaathiri mshikamano wa kisiasa wa eneo hilo na huenda ukawa na athari kwa viongozi wa Mlima Kenya katika mustakabali wa siasa za kitaifa.
Hadi sasa, Gachagua hajajibu rasmi madai ya Wamatinga wala kutoa msamaha kama alivyotakiwa. Wakati ukikaribia kumalizika kwa muda aliopewa, macho yote yanaelekezwa kwake ili kuona iwapo atatoa msamaha au hali hii itachukua mkondo wa kisheria.