
TUME ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC, imetoa notisi ya kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua ikimtaka kusitisha matamshi yanayoweza kuzua taharuki humu nchini.
Katika barua hiyo iliyotiwa saini na mwenyekiti wa NCIC
Samuel Kobia, tume hiyo ilimkaanya Gachagua dhidi ya matamshi ya uchochezi
anapoendeleza harakati zake za kuikosoa serikali ya aliyekuwa bosi wake,
William Ruto.
Kwa mujibu wa NCIC, wamebaini kwamba Gachagua alitoa Kauli zenye
utata kaunti ya Meru alipomtishia rais Ruto kutokanyaga eneo hilo ikiwa jaji
mkuu Martha Koome atabanduliwa.
“Gachagua ulitoa matamshi ambayo yana uwezekano wa kuathiri kuishi kwa usawa na amani miongoni mwa jamii mbalimbali nchini Kenya. Jumapili ya Februari 23, 2025 katika kanisa la AIPCA Antubetwe Kiongo, Igembe Kaskazini katika kaunti ya Meru, ulitoa tamko ambalo linalochukuliwa kupandisha hisia kwa sehemu ya watu wa jamii ya Ameru,” NCIC ilisema huku ikinukuu matamshi ya Gachagua.
NCIC pia ilimkosoa Gachagua kwa Kauli yake kwamba rais Ruto
ana njama ya kumbandua Martha Koome ofisini kama jaji mkuu kwa misingi ya jamii
anayotoka, Kauli ambayo waliitaja kama ya kupotosha.
“Kauli yako ya kumuonya rais Ruto kutokanyaga Meru ikiwa jaji
mkuu Martha Koome atabanduliwa ofisini ni uhujumu wa haki yake kama ishara ya
umoja wa kitaifa kuzuru kila eneo la nchi na kutekeleza majukumu yake kama rais
aliyechaguliwa na wakenya.”
Katika misingi hiyo, tume hiyo ilimtaka Gachagua kukoma mara
moja kueneza Kauli za aina hiyo.