logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Vurugu zazuka Roysambu huku polisi wakikabiliana na vijana waliotaka kuvamia kanisa la Jesus Winner

Polisi waliingilia kati haraka, wakitumia gesi ya machozi kutawanya umati uliokuwa unakusanyika.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri09 March 2025 - 15:05

Muhtasari


  • Mvutano mkali ulizuka katika mtaa wa Roysambu, kaunti ya Nairobi Jumapili baada ya kundi la vijana wenye hasira kukabiliana na polisi.
  • Mpango wa kuvamia kanisa hilo ulikuwa umesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii kupitia alama ya reli #OccupyJesusWinner.

Vurugu zilizuka Roysambu mnamo Machi 9, 2025.

Mvutano mkali ulizuka katika mtaa wa Roysambu, kaunti ya Nairobi Jumapili baada ya kundi la vijana wenye hasira kukabiliana na polisi wakijaribu kuvamia kanisa la Jesus Winner Ministry.

 Ghasia hizo zilitokana na uamuzi wa kanisa hilo kukubali mchango wa KSh 20 milioni kutoka kwa Rais William Ruto, hatua ambayo ilizua ghadhabu miongoni mwa baadhi ya vijana.

 Kwa kutarajia hali ya taharuki, usalama uliimarishwa katika eneo la kanisa, lakini waandamanaji walianza kukusanyika katika mizunguku iliyo karibu, wakionekana kujiandaa kuelekea katika kanisa hilo.

Polisi waliingilia kati haraka, wakitumia gesi ya machozi kutawanya umati uliokuwa unakusanyika. Hatua hiyo ilisababisha waandamanaji kukimbia ovyo huku machafuko yakizuka.

 Mpango wa kuvamia kanisa hilo ulikuwa umesambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii kupitia alama ya reli #OccupyJesusWinner, huku waandalizi wakiahidi kuchukua udhibiti wa kanisa kama njia ya kuonyesha kutoridhika kwao.

 Zaidi ya maandamano hayo, baadhi ya watu wenye ghadhabu walichagua kutuma jumbe za matusi kwa Askofu wa Jesus Winner Ministry, Edward Mwai, wakielezea kutoridhishwa kwao na uamuzi wa kanisa kukubali mchango huo.

 Polisi waliendelea kuwa macho siku nzima ili kuzuia vurugu zaidi.

 Awali, askofu Edward Mwai wa Kanisa la Jesus Winner Ministry alisema kwamba amewasamehe wote waliomshambulia katika kipindi cha juma moja lililopita kufuatia mchango aliopokea kutoka kwa Rais William Ruto Jumapili iliyopita..

 Akizungumza wakati wa ibada katika kanisa lake la Roysambu asubuhi ya Jumapili, kiongozi huyo wa kidini alidai kuwa wale waliokuwa wakimshambulia walikuwa wanatumiwa na watu fulani ambao anawafahamu.

 Hata hivyo, alisisitiza kuwa ameacha kila kitu mikononi mwa Mungu, akieleza kuwa yeye hapambani na mtu yeyote.

 "Yeyote amesema neno lolote mbaya. Ninasema nikiwa katika haya madhabahu, ile mawe yote amenitupia, Mungu awasamehe. Mimi nimewasamehe lakini nimewachia Mungu. Sipambani na mtu yeyote," alisema Mwai.

 Askofu huyo alidai kuwa kulikuwa na kundi la watu waliotumwa katika kanisa lake Jumapili asubuhi, na baadhi yao walinaswa wakiwa na simu.

 Hata hivyo, alisema kuwa kwa roho ya msamaha, aliomba waachiliwe.

 "Lakini watu watakuja kujua kuna Mungu kwa haya madhabahu. Kuna Mungu. Mnanishika. Yule Mungu aliongea hapa akasimamisha maombi Mombasa, huyo Mungu, watajua kuna Mungu mbinguni," alionya.

 Mwai alizungumza baada ya wiki moja ya mashambulizi makali kutoka kwa Wakenya kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mchango wa Shilingi milioni 20 aliopokea kutoka kwa Rais William Ruto mnamo Machi 2, 2025.

 Makumi ya maafisa wa polisi walipelekwa katika Kanisa la Jesus Winner Ministry, mtaa wa Roysambu, Nairobi, siku ya Jumapili baada ya vijana kadhaa kutishia kuingia kwa nguvu.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved