
Askofu Edward Mwai wa Kanisa la Jesus Winner Ministry amesema kwamba amewasamehe wote waliomshambulia katika kipindi cha juma moja lililopita kufuatia mchango aliopokea kutoka kwa Rais William Ruto Jumapili iliyopita..
Akizungumza wakati wa ibada katika kanisa lake la Roysambu asubuhi ya Jumapili, Machi 9, kiongozi huyo wa kidini alidai kuwa wale waliokuwa wakimshambulia walikuwa wanatumiwa na watu fulani ambao anawafahamu.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa ameacha kila kitu mikononi mwa Mungu, akieleza kuwa yeye hapambani na mtu yeyote.
"Yeyote amesema neno lolote mbaya. Ninasema nikiwa katika haya madhabahu, ile mawe yote amenitupia, Mungu awasamehe. Mimi nimewasamehe lakini nimewachia Mungu. Sipambani na mtu yeyote," alisema Mwai.
Askofu huyo alidai kuwa kulikuwa na kundi la watu waliotumwa katika kanisa lake Jumapili asubuhi, na baadhi yao walinaswa wakiwa na simu.
Hata hivyo, alisema kuwa kwa roho ya msamaha, aliomba waachiliwe.
"Lakini watu watakuja kujua kuna Mungu kwa haya madhabahu. Kuna Mungu. Mnanishika. Yule Mungu aliongea hapa akasimamisha maombi Mombasa, huyo Mungu, watajua kuna Mungu mbinguni," alionya.
Mwai alizungumza baada ya wiki moja ya mashambulizi makali kutoka kwa Wakenya kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mchango wa Shilingi milioni 20 aliopokea kutoka kwa Rais William Ruto mnamo Machi 2, 2025.
Makumi ya maafisa wa polisi walipelekwa katika Kanisa la Jesus Winner Ministry, mtaa wa Roysambu, Nairobi, siku ya Jumapili baada ya vijana kadhaa kutishia kuingia kwa nguvu.
Ruto alilisifu kanisa la Mwai kwa kuandaa zoezi la uandikishaji wa vijana kwa mpango wa serikali unaolenga kuwaunganisha na fursa za ajira nje ya nchi.
"Tunashukuru Kanisa la Jesus Winner Ministry kwa kusaidia Mpango wetu wa Uhamaji wa Kazi kwa kuwaandikisha vijana kwa ajili ya kupata ajira nje ya nchi," alisema Ruto.
"Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi tunapopanua fursa za ajira na kipato kwa vijana wetu."