
Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, mnamo siku ya Jumapili alikumbana na mapokezi mabaya katika Uwanja wa Gusii katika kaunti ya Kisii alipohudhuria hafla ya kandanda.
Raila alikuwa amezuru Kisii kwa ajili ya kushudia kutiwa saini mkataba wa udhamini wa Sportspesa na Shabana FC, ingawa hakuwa na hakika kama angepokewa vizuri.
Mara tu Waziri Mkuu huyo wa zamani aliposimama kuhutubia mashabiki, sehemu ya umati ilianza kumzomea kwa kauli ya "Raila must go!"
Wengine walionyesha kutoridhishwa kwa kuondoka uwanjani.
Hata hivyo, Raila aliendelea na hotuba yake bila kuyumbishwa
na malalamiko hayo.
Hatua hii inaonekana kuchochewa na hatua ya ODM kusaini makubaliano (MoU) na chama cha UDA cha Rais William Ruto—uamuzi ambao umewaghadhabisha baadhi ya viongozi na wafuasi wa ODM.
Eneo la Kisii kwa muda mrefu limekuwa likichukuliwa kama ngome
ya Raila, jambo linalofanya tukio hili kuwa la kipekee.
Hatua ya kusaini makubaliano hayo ilitanguliwa na mashauriano ya Raila na wanachama wa chama chake katika ngome zake za kisiasa, akitafuta maoni kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa.
Wiki iliyopita, kinara huyo wa ODM na rais William Ruto waliingia rasmi katika makubaliano ya kisiasa yatakayoshuhudia vyama vyao vikishirikiana.
Mkataba wa Ushirikiano kati ya Kenya Kwanza na ODM ulisainiwa Ijumaa katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, kwenye hafla iliyohudhuriwa na Wabunge wanaomuunga mkono kila kiongozi.
Naibu Rais Kithure Kindiki pia alihudhuria hafla hiyo.
Kupitia mkataba huu, vyama vya UDA na ODM vitashirikiana katika masuala ya kitaifa kwa kutumia miundombinu yao ya kisiasa.
Pia, vyama hivyo vitawatumia wataalamu wao mahiri kwa mashauriano kuhusu utawala na sera za kitaifa.
Kabla ya hafla ya utiaji saini, maelfu ya wafuasi wa ODM walikusanyika katika KICC kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Hafla hiyo ilifuatia mfululizo wa mashauriano ambayo kiongozi wa ODM Raila Odinga alifanya katika maeneo mbalimbali nchini ambako ana uungwaji mkono mkubwa wa kisiasa.