
RAIS William Ruto amemsifia kiongozi wa upinzani Raila Odinga kama mtu ambaye amejitolea mara si moja kuona amani na umoja katika taifa hili.
Mkuu wa nchi alitoa Kauli hii ya shukrani dakika chache baada
ya wawili hao kutia saini mkataba wa makubaliano ya kufanya kazi pamoja kati ya
ODM na UDA.
Ruto alisema kwamba historia ya taifa la Kenya itamhukumu
Odinga kwa njia nzuri kwa kuzingatia vitu ambavyo amepitia na jinsi ambavyo
amekuwa akiweka suala la amani mbele kuliko masuala mengine.
“Ni sharti nimhongere
Raila Odinga na ujasiri anao kufanya maamuzi magumu. Sio viongozi wengi wenye
ujasiri wa kuweka masuala ya taifa mbele ya maslahi yao binafsi na nasema hilo
bila kutetereka,” Ruto alisema.
“Ninajua aina ya ugumu
ambao ndugu yangu mkubwa [Raila] amepitia hadi kutufikisha katika nafasi hii. Na
ndugu yangu Odinga historia itaenda kukuhukumu kwa njia nzuri kwa kile ambacho
umefanyia hili taifa,” Ruto aliongeza.
Kiongozi wa taifa alirejelea Kauli yake aliyomwambia Raila
Odinga siku kadhaa baada ya kumshinda katika uchaguzi wa urais 2022,
akimhakikishia kwamba atamtunza vyema.
“Siku kadhaa baada ya
uchaguzi, niliongea na ndugu yangu Raila Odinga na nikamwambia, wewe umekuwa
kiongozi wangu wa chama, na umekuwa mkubwa wangu, leo kwa neema ya Mungu mimi
ndiye rais, ninataka utunzwe vizuri. Na nitafanya chochote kadri ya uwezo wangu
kuhakikisha kwamba unaheshimiwa Kenya,” Ruto alimuahidi Raila.
Akiwatoa wasiwasi wenye dhana kwamba anafanya hivyo kwa
kujifaidi mwenyewe, rais Ruto alisema kwamba atafanya hivyo kwa sababu anaamini
mkongwe huyo wa siasa anastahili.
“Sifanyi hivi kwa sababu
nyingine yoyote ya kunifaidi mimi. Ninafanya hivi kwa sababu mimi ni mdogo
kiumri ikilinganishwa na Raila na pia ninaelewa kwamba yeye ni mtu mkubwa na mchanga
wake kwa Kenya unastahili heshima,” alifafanua.
Vyama vya UDA na ODM vilikongamana katika ukumbi wa KICC mchana
wa Machi 7 na kutia saini mkataba wa kufanya kazi pamoja.
ODM na UDA sasa watagawana nafasi za uongozi serikalini
miongoni mwa faida zingine zitakazotokana na makubaliano hayo.