
Rais William Ruto, ameendelea kuongoza juhudi za kurejesha amani nchini Sudan Kusini kwa kusisitiza mazungumzo kama suluhisho la mgogoro unaoendelea.
Hali ya usalama katika taifa hilo changa barani Afrika imeendelea kuzorota, na hivyo kuibua wasiwasi mkubwa katika eneo zima la Afrika Mashariki.
Mnamo Alhamisi, Machi 6, Rais Ruto alisema alizungumza na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit, pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar, kuhusu hali ya usalama inayozidi kuzorota nchini humo.
"Niliwasihi viongozi wote wawili kushiriki katika mazungumzo yenye lengo la kuleta amani nchini mwao, huku eneo hili likiendelea kufanya juhudi za kuleta uthabiti Sudan Kusini chini ya Mkakati wa Kistratejia wa IGAD," alisema Rais Ruto katika taarifa rasmi iliyotolewa na Ikulu ya Nairobi.
Aidha, Rais Ruto alifichua kuwa mashauriano ya kieneo yanaendelea kufanyika ili kubaini njia mwafaka ya kusuluhisha mgogoro wa Sudan Kusini.
Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo Desemba 2013 baada ya mzozo wa kisiasa ndani ya chama tawala cha Sudan People's Liberation Army (SPLA).
Tofauti za kisiasa kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wake wa wakati huo, Riek Machar, zilichochea mapigano yaliyoenea kwa kasi na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha huku wengine wakikimbilia mataifa jirani kama wakimbizi.
Licha ya juhudi mbalimbali za kuleta amani kupitia makubaliano ya kusitisha mapigano mnamo 2015, 2017, 2018 na 2024, hali ya kutoelewana imeendelea kushuhudiwa.
Katika hatua za kusuluhisha mzozo huo, Kenya ilianzisha mpango wa mazungumzo wa Tumaini Initiative, ulioanzishwa Nairobi.
Mazungumzo haya yalirejelewa Novemba 2024 baada ya kusimama kwa miezi mitatu.
Mpango huu unahusisha makundi ya waasi ambayo hayakusaini Mkataba wa Juba wa 2018, na unalenga kuwahusisha wadau wote wa kisiasa ili kufanikisha amani ya kudumu.
Baadhi ya makundi ya waasi yaliyotia saini makubaliano hayo ni Sudan Liberation Army Movement (wingi la Arko Minawi), Justice and Equality Movement, na kundi la Malik Aqar, miongoni mwa mengine.
Mpango wa Nairobi Tumaini Initiative unalenga kuunga mkono juhudi za IGAD katika kuhakikisha utekelezaji wa mkataba wa Revitalized Agreement on the Resolution of the Conflict in South Sudan, ili taifa hilo lipate amani ya kudumu.
Mgogoro wa Sudan Kusini umeathiri siyo tu wananchi wa taifa hilo, bali pia mataifa jirani kama Kenya, Uganda na Ethiopia, ambayo yamepokea maelfu ya wakimbizi wanaotoroka mapigano. Uchumi wa Sudan Kusini, ambao unategemea mafuta, umedorora huku miundo mbinu ikiharibiwa kutokana na vita.
Juhudi za Rais Ruto na mataifa ya Afrika Mashariki zinaonyesha dhamira ya kuleta uthabiti katika eneo hili. Kupitia mashauriano ya kieneo na ushirikiano wa IGAD, kuna matumaini kwamba mgogoro huu utapatiwa suluhu la kudumu.