
Mvutano kati ya Kenya na Sudan bado unaendelea kutokota haswa baada ya wanamgambo wa RSF kutangaza wapo mji mkuu wa Nairobi.
Katika mtafaruku huu serikali ya kijeshi ya Sudan imemtangua balozi wake nchini Kenya, kwa kulalamikia uamuzi wa Nairobi kuwakubalia wanamgambo wa RSF pamoja na vikundi vinavyoshirikiana nao kuanzisha mkataba wa kisiasa unaolenga kuunda serikali mbadala katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo.
Haya yanajiri kukiwa na siutafahamu iwapo RSF wataendelea na mkutano wake leo, baada ya kuahirisha vikao na wanahabari Alhamisi.Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Sudan, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilisema kuwa imemuita Balozi Kamal Jabbara kwa mashauriano kutoa malalamiko kuhusu hatua ya Kenya ya kuwa mwenyeji wa wanamgambo hao.
Sudan inalaumu Kenya kwa kudai kuwa imekiuka majukumu yake ya kimataifa kwa kuwapokea viongozi wa RSF, akisema kuwa hii ni hatua inayosababisha mgawanyiko mkubwa katika mchakato wa kisiasa wa kanda hiyo.
Serikali ya Kenya ilijibu kwa kujitetea, ikisema kuwa ilitoa tu jukwaa la kimsingi kwa ajili ya mazungumzo, ikifuata utamaduni wake wa muda mrefu wa kusaidia mazungumzo na majadiliano ya amani katika muktadha wa kisiasa wa Mashariki ya Afrika.
Hata hivyo, Sudan iliongeza lawama yake kwa kusema kuwa Kenya imekuwa ikitoa msaada wa vifaa na rasilimali kwa RSF, na kilele ikiwa kuwapa fursa ya kutia saini mkataba wanaoutaja utagawanya nchi.
Pia, Sudan ilidai kuwa Kenya ni sehemu ya “njama ya kuunda serikali mbadala” na kumkosoa vikali Rais William Ruto kwa kutilia mkazo maslahi yake binafsi na ya kibiashara na kiongozi wa RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, badala ya kuzingatia uhusiano wa kihistoria wa Sudan na Kenya, ambao unahusisha ushirikiano wa muda mrefu.
Hii ni mara ya pili mwaka huu ambapo Sudan imemtangua balozi wake nchini Kenya kutokana na uhusiano wa nchi hiyo na Jenerali Dagalo. Mnamo mwezi Januari, Sudan ilikosoa rasmi hatua ya Kenya kumpokea kiongozi huyo wa RSF kwa heshima ya kitaifa.