
Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga
wamekubaliana juu ya mfumo wa kazi wa pamoja unaolenga kushughulikia changamoto
kuu za kijamii, kiuchumi, na kisiasa nchini Kenya.
Katika Mkataba wa Maelewano (MoU), viongozi hao wametaja maeneo kumi ya kipaumbele, huku utekelezaji kamili wa ripoti ya NADCO ukiwa wa kwanza.
Hii inajumuisha kupunguza gharama ya maisha, kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, na kuunda mfumo wa utekelezaji wa sheria ya jinsia mbili-thuluthi.
Kujumuisha Wote na Kulinda Ugatuzi
Ruto na Raila wamehimiza ushirikishwaji mkubwa wa wananchi katika masuala ya umma, wakikiri kuwa licha ya katiba kutambua haki za makundi yaliyo pembezoni, utekelezaji wake bado ni dhaifu takriban miaka 15 baada ya kupitishwa kwake.
"Kenya ni ya kila Mkenya bila kujali kabila, dini, kizazi, au eneo. Kila raia anastahili mgao wa rasilimali kwa usawa na fursa sawa katika uteuzi wa umma," MoU inasema.
Viongozi hao pia wameahidi kulinda ugatuzi dhidi ya changamoto
zozote zinazoweza kudhoofisha mamlaka ya kaunti. Wamelenga kuhakikisha kuwa
fedha zote zinazotengwa kwa shughuli zilizopelekwa kaunti zinatolewa kwa wakati
na bila masharti.
Uwezeshaji wa Vijana na Mageuzi ya Kiuchumi
Mkataba huo unasisitiza uwekezaji mkubwa katika sekta zenye uwezo wa juu kama kilimo, TEHAMA, madini, na uchumi wa bahari.
Kwa lengo la kubuni ajira endelevu, viongozi hao wanapendekeza mipango ya kiuchumi ya kitaifa na kuhakikisha kuwa vijana wanapata nafasi za kushiriki kikamilifu katika uongozi na siasa. "Vijana lazima wahusishwe moja kwa moja katika shughuli zote za kitaifa," nyaraka hiyo inasema.
Utawala, Maadili ya Umma, na Haki ya Maandamano
Ruto na Raila wanakiri kuwa wananchi wamekerwa na mienendo ya baadhi ya maafisa wa serikali wanaoonyesha utajiri wa kupindukia huku wakidhihaki raia. Ili kurejesha heshima, wanapendekeza maafisa wa umma wazingatie nidhamu na uwajibikaji, pamoja na kuweka sheria kali dhidi ya mgongano wa maslahi.
Katika suala la maandamano ya amani, viongozi hao wanataka
kuboreshwa kwa mbinu za polisi za kudhibiti maandamano, kufidiwa kwa waathiriwa
wa ukiukwaji wa haki, na kusamehewa kwa wale waliokamatwa kwa kushiriki
maandamano ya amani.
Kudhibiti Deni la Taifa na Kupambana na Ufisadi
MoU hiyo pia inataka kufanyika kwa ukaguzi wa kina wa historia ya madeni ya Kenya ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji. "Mikopo ya taifa lazima isimamiwe kwa uwazi, na kila shilingi inayokopwa ihesabiwe," inasema.
Kuhusu ufisadi, viongozi hao wanataka hatua madhubuti badala ya maneno matupu. Wanasema taasisi za uwajibikaji kama Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mdhibiti wa Bajeti, na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi lazima ziimarishwe.
Kuongeza Ufanisi wa Serikali na Utawala wa Sheria
Mkataba huo unasema ni muhimu kupunguza matumizi mabaya ya fedha za umma na kuhakikisha kuwa matumizi ya serikali yana tija katika ngazi zote.
"Demokrasia haiwezi kustawi ikiwa vyama vya siasa vinadhoofishwa, uhuru wa kujieleza unabanwa, au utawala wa sheria unakiukwa," MoU inasema.
Ruto na Raila pia wameahidi kuheshimu Sheria ya Vyama vya
Kisiasa na kulinda uhuru wa vyama vyote vya kisiasa nchini.