
Seneta wa Kisii, Richard Onyonka, amekanusha vikali madai ya kudhamini maandamano dhidi ya kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, yaliyofanyika katika Uwanja wa Gusii mnamo Machi 9, 2025.
Madai haya yalitolewa na mtumiaji mmoja wa mtandao wa Facebook ambaye alidai kuwa Onyonka na ndugu yake, Kibagendi, walihusika katika kupanga uhasama dhidi ya kiongozi wa ODM.
Katika taarifa yake siku ya Jumapili jioni, Onyonka alieleza kuwa wakati wa tukio hilo, alikuwa jijini Mombasa kwa shughuli za kikazi, huku ndugu yake Kibagendi akiwa pia na majukumu mengine nje ya Kisii.
"Niko Mombasa kwa kazi, na ndugu yangu Kibagendi pia yuko nje kwa majukumu ya kikazi. Ni upuuzi mkubwa kwa mtu yeyote kutuhusisha sisi na yaliyotokea katika Uwanja wa Gusii leo," Onyonka alisema kupitia mtandao wa X.
Seneta huyo alisisitiza kuwa haiwezekani kwa mtu binafsi kuhamasisha au kulipa zaidi ya mashabiki 15,000 wa soka kuhudhuria mechi, kwani wamekuwa wakifanya hivyo kwa kujitolea bila ushawishi wa mtu yeyote.
Aliongeza kuwa mashabiki wa Shabana wanajulikana duniani kote kwa kusapoti timu yao bila masharti, na ni dharau kwao kudai kuwa wanalipwa kuhudhuria mechi.
"Matukio yaliyotokea Kisii mchana huu ni ya kusikitisha. Hata hivyo, hii inapaswa kuwa mwito wa kuamsha kwa wahusika husika kuchunguza na kujua kwa nini watu wanapinga Baba Raila Odinga katika Kisii." aliongeza.
Seneta huyo alibainisha kuwa katika zaidi ya miongo miwili ya siasa, hajawahi kuhusishwa na vurugu au machafuko, na wapiga kura wake wanaweza kuthibitisha hilo.
“Ninapinga kutovumiliana kisiasa na nawasihi watu wetu kutenda kwa kujizuia na busara siku zijazo," alisema.
Siku ya Jumapili, kiongozi wa ODM, Raila Odinga alipata mapokezi mabaya katika Uwanja wa Gusii katika kaunti ya Kisii alipohudhuria hafla ya kandanda.
Raila alikuwa amezuru Kisii kwa ajili ya kushudia kutiwa saini mkataba wa udhamini wa Sportspesa na Shabana FC, ingawa hakuwa na hakika kama angepokewa vizuri.
Mara tu Waziri Mkuu huyo wa zamani aliposimama kuhutubia mashabiki, sehemu ya umati ilianza kumzomea kwa kauli ya "Raila must go!" Wengine walionyesha kutoridhishwa kwa kuondoka uwanjani.
Hata hivyo, Raila aliendelea na hotuba yake bila kuyumbishwa na malalamiko hayo.
Hatua hii inaonekana kuchochewa na hatua ya ODM kusaini makubaliano (MoU) na chama cha UDA cha Rais William Ruto—uamuzi ambao umewaghadhabisha baadhi ya viongozi na wafuasi wa ODM.
Eneo la Kisii kwa muda mrefu limekuwa likichukuliwa kama ngome ya Raila, jambo linalofanya tukio hili kuwa la kipekee.
Hatua ya kusaini makubaliano hayo ilitanguliwa na mashauriano ya Raila na wanachama wa chama chake katika ngome zake za kisiasa, akitafuta maoni kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa.