
Maafisa wa polisi wamemkamata washukiwa watatu katika eneo la Nyabisimba, Kaunti ya Nyamira, kwa tuhuma za kumshambulia mwanamke wakati wa mazishi ya mumewe wa zamani.
Washukiwa hao wanadaiwa kumlazimisha mwanamke huyo kushiriki katika mila za kitamaduni, kinyume na matakwa yake, kabla ya kumvamia na kumsababishia majeraha mwilini.
Tukio hilo linaripotiwa kutokea mnamo Machi 21, 2025, wakati mwanamke huyo aliyekuwa ameolewa na marehemu kwa zaidi ya miaka tisa, aliwasili kwenye mazishi yake kufuatia mwaliko wa mama mkwe wake.
Mwanamke huyo alikuwa ametengana na marehemu kwa muda mrefu na hakuwa na mawasiliano naye hadi alipofariki dunia katika ajali ya barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, hali ilibadilika ghafla wakati wa mazishi, baada ya baadhi ya jamaa wa marehemu kumtaka atimize desturi ya kutupa mchanga kaburini.
Mwathiriwa alipokataa, inadaiwa kuwa walimshutumu kwa kusababisha kifo cha mumewe wa zamani na kisha wakamshambulia vikali mbele ya waombolezaji.
Maafisa wa polisi walifahamishwa kuhusu tukio hilo na kuanzisha msako mara moja.
Hatimaye, washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Mwongorisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kiambere kwa uchunguzi zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, juhudi za kuwatambua na kuwakamata washukiwa wengine wanaohusishwa na shambulio hilo zinaendelea.