Kampuni ya mabasi ya Super Metro imevunja kimya chake kufuatia ajali iliyohusisha basi lake lenye nambari ya usajili KDL 360F, iliyotokea asubuhi ya Jumamosi, Machi 29, 2025, katika eneo la Jomoko, barabara ya Thika.
Katika taarifa yake kwa umma siku ya Jumamosi, kampuni hiyo ilitangaza kuwa hakuna majeruhi wala vifo vilivyoripotiwa kutokana na ajali hiyo.
Kwa mujibu wao, ajali hiyo ilisababishwa na gari dogo jeupe la saloon ambalo lilikuwa limepakia mizigo ya Muratina kupita kiasi, na dereva wake alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kuyumba, jambo ambalo liliwashangaza madereva wengine waliokuwa barabarani.
"Gari hilo liligonga upande wa basi letu, jambo lililomlazimu dereva wetu kuchukua hatua za dharura ili kuepuka kugongana vibaya. Kwa bahati mbaya, basi letu likaelekezwa nje ya barabara na kutumbukia kwenye mtaro," ilisoma sehemu ya taarifa hiyo.
Super Metro imeeleza kuwa mara baada ya ajali hiyo, waliripoti suala hilo kwa mamlaka husika, ambapo Kituo cha Polisi cha Thika kwa sasa kinaendelea kuchunguza chanzo kamili cha ajali hiyo.
Wamesisitiza kuwa yeyote anayehitaji maelezo rasmi kuhusu tukio hilo anapaswa kuwasiliana na polisi kwa taarifa sahihi na zilizosasishwa.
Mnamo siku ya Jumamosi asubuhi, abiria waliokuwa ndani ya basi moja la kampuni ya Super Metro walinusurika bila majeraha baada ya ajali kutokea kwenye Barabara ya Thika.
Ilihusisha basi la Super Metro na gari binafsi, ambapo basi hilo liligonga gari hilo kisha kupinduka barabarani, huku gari dogo likitumbukia mtaroni.
Mashahidi na maafisa wa polisi waliripoti kuwa ingawa baadhi ya abiria walipatwa na mshtuko, hakuna aliyeripotiwa kujeruhiwa.
Video iliyosambaa mtandaoni ilionyesha wapita njia wakijitahidi kuwaokoa waliokuwa ndani ya basi hilo lililopinduka.
Ajali hiyo ilisababisha msongamano wa magari katika njia ya kushukisha abiria wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.
Maafisa wa polisi wamethibitisha kuwa uchunguzi umeanzishwa ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.