logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Sudi awasifia wakazi wa Nyeri kwa mapokezi ya kipekee kwa Rais Ruto

Kupitia taarifa baada ya ziara hiyo, Sudi alieleza kuvutiwa na shauku na dhamira waliyoonyesha wakazi wa Nyeri.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri02 April 2025 - 10:14

Muhtasari


  • Kwa mujibu wa Sudi, wakazi wa Nyeri wamedhihirisha nia yao ya kuacha migawanyiko ya kisiasa na kuangazia maendeleo.
  • Sudi, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Gachagua, amekuwa akizozana mara kwa mara na viongozi wanaomuunga mkono Gachagua.

Oscar Sudi na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga

Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, amewapongeza wakazi wa Nyeri kwa kujitokeza kwa wingi kumkaribisha Rais William Ruto wakati wa ziara yake siku ya Jumanne.

Kupitia taarifa baada ya ziara hiyo, Sudi, aliyekuwa ameandamana na Rais pamoja na Naibu Rais Kithure Kindiki na viongozi wengine, alieleza kuvutiwa na shauku na dhamira waliyoonyesha wakazi wa Nyeri.

Kwa mujibu wa Sudi, wakazi wa Nyeri—kaunti anayotoka aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua—wamedhihirisha nia yao ya kuacha migawanyiko ya kisiasa na kuangazia maendeleo.

Mbunge huyo aliwasifu kwa kuweka mbele umoja, bidii, na maendeleo badala ya migogoro na siasa za ukabila.

“Nimevutiwa sana na idadi kubwa ya watu waliokuja na ari yao ya kujituma. Mmeamua kuachana na migawanyiko midogo na kujikita katika kujenga maisha bora kupitia bidii na maendeleo.

“Wakati wengine wanapanda mbegu za mgawanyiko na siasa za kikabila, ninyi mmechagua umoja na maendeleo ya pamoja. Asante sana, Nyeri,” Sudi alisema.

Sudi, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Gachagua, amekuwa akizozana mara kwa mara na viongozi wanaomuunga mkono Gachagua, huku akijihusisha na malumbano makali mtandaoni.

Kauli yake ilijiri wakati Rais Ruto alianza ziara ya maendeleo ya wiki moja katika eneo la Mlima Kenya, ziara ambayo hapo awali ilikuwa imeibua hisia mseto kuhusu jinsi angepokelewa.

Ziara hiyo ilianza Laikipia Jumanne, ambapo Rais alizindua miradi kadhaa ya maendeleo. Hatimaye alihitimisha siku hiyo Nyeri, akihutubia umati mkubwa katika Narumoru.

Katika eneo la Mwicwiri, Ruto alizindua Mpango wa Last Mile Connectivity wenye thamani ya Sh850 milioni, ambao utaunganisha nyumba 10,000 kaunti ya Nyeri na umeme. Pia alitangaza kutengwa kwa Sh550 milioni zaidi ili kuhakikisha kila mkazi wa kaunti hiyo anapata umeme.

Kiongozi wa nchi pia alizindua jengo jipya lenye ghorofa moja na madarasa 12 katika Shule ya Msingi ya Narumoru Township na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Soko la Narumoru, linalotarajiwa kukamilika ndani ya mwezi mmoja.

Katika kipindi chote cha ziara yake ya Mlima Kenya, Rais Ruto atakuwa akihudumu kutoka Ikulu ndogo ya Sagana, kaunti ya Nyeri.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved