logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Gachagua azungumzia alivyofadhili safari ya urais ya Ruto

Gachagua alifichua kuwa uamuzi wake wa kumfadhili Ruto kifedha ulimuingiza matatani na serikali ya awali.

image
na Samuel Mainajournalist

Yanayojiri08 April 2025 - 10:10

Muhtasari


  • Gachagua amedai kuwa alifadhili kwa kiwango kikubwa kampeni za Rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
  • Gachagua alisema alifadhili kampeni hizo kutokana na kujitolea kwake binafsi na hakuwa na nia ya kudai fedha yoyote.

Rigathi Gachagua

Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua amedai kuwa alifadhili kwa kiwango kikubwa kampeni za Rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza katika mahojiano na KTN jioni ya Jumatatu, Gachagua—aliyeondolewa madarakani mwaka jana baada ya kutofautiana na Rais—alifichua kuwa uamuzi wake wa kumfadhili Ruto kifedha ulimuingiza matatani na serikali ya awali.

"Nilijikuta matatani na serikali ya awali kwa sababu nilikuwa nafadhili kampeni za Ruto," alisema Gachagua.

Naibu kiongozi huyo wa zamani wa UDA alikuwa akijibu madai kwamba alidai Ksh10 bilioni kutoka kwa Rais kabla ya kuondolewa madarakani.

Huku akifafanua zaidi, Gachagua alisema alifadhili kampeni hizo kutokana na kujitolea kwake binafsi na hakuwa na nia ya kudai fedha yoyote.

“Walifungia akaunti zangu, wakazuia biashara zangu, na wakajaribu kunizuia. Niliwekeza sana katika kampeni yake—mimi si mtu wa kumzunguka nikimwomba pesa,” alisema.

Wakati huohuo, Gachagua alikanusha madai kwamba alijaribu kumshawishi Rais William Ruto kwa kumtaka ampe Shilingi bilioni 10.

Madai hayo yaliibuka mwezi Machi wakati Rais Ruto, katika mahojiano na vyombo vya habari mjini Nyeri, alidai kwamba Gachagua alimtaka kiasi hicho cha fedha ili kusaidia kuimarisha uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya.

Hata hivyo, Gachagua, alisisitiza kwamba ana mali za kutosha na hahitaji fedha kutoka kwa Rais.

“Rais hakuzungumza kuhusu madai ya kunishinikiza hadi alipofika Mlima Kenya,” alisema Gachagua. “Kama kweli ningemshinikiza, hilo lingekuwa shtaka la kwanza katika hoja ya kuniondoa madarakani Bungeni—halikuwepo. Kumlazimisha mtu ni kosa la jinai,” Gachagua alisema.

Gachagua aliongeza kuwa wakati Ruto alitembelea eneo la Magharibi mwa Kenya, alihusisha kutofautiana kwao na masuala ya kutojali na ukabila, si kwa madai ya rushwa.

“Alipokuwa Magharibi, alisema aliniachisha kazi kwa sababu mimi si mweledi na ni wa kikabila. Hakuwambia kwamba nilimtaka Shilingi bilioni 10,” alisema.

Akijitetea kuhusu hali yake ya kifedha, Gachagua alisema amejijengea utajiri wake kupitia biashara nyingi kwa miaka mingi, na hahitaji msaada wa kifedha kutoka kwa mtu yeyote.

“Mimi si mtu wa kumwomba Rais pesa, na yeye anajua hilo. Mimi ni mfanyabiashara hodari ambaye nimefanya kazi kwa miaka mingi. Nilijiunga na kampeni kwa hiari yangu. Hakunilazimisha. Nilitumia pesa zangu kwa sababu niliamini katika jambo hilo. Pia nilisaidiwa na marafiki,” alieleza.

Alisisitiza kuwa kama kweli alitoa ombi hilo, Rais angekuwa amelizungumza miezi sita iliyopita.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved