
Serikali ya Marekani imethibitisha upya uungwaji mkono wake kwa kikosi cha kimataifa cha usalama kinachoongozwa na Kenya nchini Haiti, pamoja na juhudi za ukanda huo kuhakikisha nchi hiyo ya Karibea inarejelea hali ya utulivu.
Hatua hiyo ilitangazwa baada ya kikao kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Mottley, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Karibea (CARICOM).
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Marekani ilisifu tamko la CARICOM linalolaani hatua zozote zinazolenga kutatiza Baraza la Rais wa Mpito nchini Haiti.
“Baada ya majadiliano kati ya Waziri na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Waziri Mkuu Mia Mottley, Marekani inaunga mkono tamko la CARICOM linalopinga vitendo vyovyote vya kuathiri uongozi wa mpito wa Haiti,” alisema msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Tammy Bruce.
Bruce aliongeza kuwa Marekani pia inaunga mkono juhudi za kikosi cha usalama kinachoongozwa na Kenya pamoja na CARICOM kusaidia serikali ya Haiti kurejesha amani na usalama miongoni mwa vitisho vinavyozidi kutoka kwa magenge yaliyojihami.
Kwa mujibu wa Bruce, Marekani inaendelea kushauriana na serikali mbalimbali za ukanda huo kuhusu hali ya usalama nchini Haiti.
Kenya kwa sasa imetuma maafisa wa polisi 800 nchini humo chini ya mpango wa MSS uliopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba 2023. Maafisa hao waliwasili rasmi mwezi Juni 2024.
Ingawa mpango huo umeidhinishwa na UN, hauendeshwi moja kwa moja na Umoja wa Mataifa bali unategemea misaada ya hiari kutoka kwa mataifa yanayounga mkono.
Haiti imekuwa ikikumbwa na misukosuko ya kisiasa kwa miaka mingi, lakini katika miezi ya hivi karibuni, ghasia zimeongezeka kwa kasi, huku ripoti zikionyesha kuwa magenge ya wahalifu yanadhibiti karibu asilimia 80 ya jiji kuu la Port-au-Prince.
Kikosi cha Kenya ni sehemu ya nguvu
kazi ya kimataifa yenye maafisa wapatao 2,500 kutoka mataifa mbalimbali.