

Msako wa kumtafuta afisa wa pili wa Kenya aliyepotea nchini Haiti bado unaendelea, huku mamlaka zikifanya juhudi za kuhakikisha anapatikana.
Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja mnamo Jumapili alithibitisha kuwa juhudi zinaendelea kumtafuta afisa huyo, aliyeripotiwa kutoweka Jumanne baada ya msafara wa Multinational Security Support (MSS) kuvamiwa na magenge ya wahalifu.
Afisa huyo alipotea wakati maafisa wa Kenya na Haiti walivamiwa walipokuwa wakisaidia gari la polisi wa Haiti lililokwama kwenye mtaro, ambao unashukiwa kuchimbwa makusudi na magenge hayo.
Akizungumza kuhusu suala hilo wakati wa maombi ya Eid katika Business Bay Square (BBS) Mall, Eastleigh, Nairobi,siku ya Jumapili Kanja aliwahakikishia Wakenya kuwa watapewa taarifa mpya punde tu maendeleo mapya yatakapopatikana.
"Tunamtafuta na hatutapumzika hadi tumempata. Tukimpata, tutawajulisha," alisema.
Hapo awali, serikali ya Haiti ilimtambulisha rasmi afisa wa Kenya aliyeuawa wakati wa shambulio hilo kuwa ni Benedict Kabiru.
Baraza la Mpito la Urais wa Haiti lilimsifu Kabiru kwa ujasiri wake na kujitolea kwake kutekeleza jukumu lake la kuleta amani.
“Baraza la Mpito la Urais lina toa rambirambi zake za dhati kwa serikali na watu wa Kenya, pamoja na familia ya Benedict Kabiru, ambaye aliangamia Machi 25 huko Savien akitekeleza jukumu lake,” ilisoma sehemu ya taarifa hiyo.
Baraza hilo lilimtaja Kabiru kuwa "shujaa aliyetoa maisha yake kwa ajili ya mustakabali bora wa Haiti" na kuahidi kuwa wahusika wa mauaji yake watakabiliwa na mkono wa sheria.
Mamlaka za Kenya tayari zimewatuma maafisa wa usalama maalum kushirikiana na vyombo husika vya Haiti katika juhudi za kurejesha mwili wa Kabiru, ambao kwa sasa ungali mikononi mwa magenge ya wahalifu.
Katika taarifa nyingine, IG Kanja amepuuza madai kwamba Marekani imesitisha ufadhili wake kwa operesheni ya MSS. Amesisitiza kuwa, licha ya maagizo mapya ya Rais Donald Trump ya kupunguza msaada wa kigeni, msaada wa kifedha kwa operesheni hiyo ya usalama Haiti haujaathirika.
Afisa Benedict Kabiru aliripotiwa kutoweka mnamo Machi 25, 2025, baada ya shambulio la genge wakati wa operesheni ya kulinda amani nchini Haiti.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Jumanne, Machi 25, 2025, na msemaji wa Mpango wa Usaidizi wa Usalama wa Kimataifa (MSS) Jack Ombaka, shambulio hilo lilitokea mnamo saa nne unusu jioni katika eneo la Pont-Sonde, jimbo la Artibonite, wakati gari la kivita la Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP) lilipokwama kwenye mtaro unaoshukiwa kuchimbwa kwa makusudi na magenge ya wahalifu.
“Tulipopokea taarifa za tukio hilo, magari mawili ya kivita ya MSS Mine-Resistant Ambush Protected (MRAP) yalitumwa kutoka Pont-Sonde kusaidia katika operesheni ya uokoaji,” taarifa hiyo ilieleza.
Hata hivyo, juhudi za kuwaokoa maafisa wa Haiti zilitatizika baada ya moja ya magari ya MSS pia kukwama, huku jingine likipata hitilafu ya kiufundi. Wakati vikosi vya uokoaji vikiendelea kushughulikia hali hiyo, washukiwa wa magenge waliokuwa wamejificha walitekeleza shambulio la kushtukiza.
Kufuatia mashambulizi hayo, afisa wa Kenya Benedict Kabiru alitowekana na Ombaka alisema vikosi maalum vilikuwa vimeanzisha msako ili kubaini aliko.
“Kufuatia tukio hili, afisa mmoja wa Kikosi cha Kenya hajulikani aliko. Timu maalum za utafutaji na uokoaji zimepelekwa kufuatilia nyayo zake na kubaini alipo,” alisema msemaji wa MSS, Jack Ombaka.
MSS iliahidi kutoa taarifa ya kina baadaye kuhusu tukio hilo na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha usalama wa maafisa wake wanaohudumu nchini Haiti.