
JACK Ombaka, msemaji wa oparesheni ya polisi wa Kenya nchini Haiti amevunja kimya kuhusu aliko polisi wa Kenya aliyetoweka wiki mbili zilizopita nchini humo Benedict Kabiru.
Katika mahojiano ya kipekee kutoka nchini
Haiti na runinga ya NTV Kenya, Ombaka alikanusha uvumi unaoendeshwa mitandaoni
kwamba Kabiru alitekwa na magenge wa Haiti na kuuawa.
Kulingana na msemaji huyo wa MSS, juhudi
za kumtafuta Kabiru bado zinaendelea na kwamba wamepiga hatua kubwa katika
kuelekea kumkomboa kutoka mikononi mwa magenge hao akiwa hai.
“Kwanza kabisa ningependa kuripoti
kwamba tumepiga hatua kubwa katika kumtafuta. Ofisa ambaye tunamzungumzia
Benedict Kabiru alihusika katika oparesheni hii na wakati huo ndio alitoweka,”
Ombaka alisema.
“Tunavyozungumza sasa hivi, bado
tunaendelea kufuatilia aliko afisa huyo, bado amesalia kutoweka lakini nina
furaha kuripoti kwamba tunatumia rasilimali zetu zote kuhakikisha tunampata na
mpaka sasa tumepiga hatua muhimu,”
aliongeza.
Kuhusu video ambayo imekuwa ikienezwa
mitandaoni ikionyesha yule anayedhaniwa kuwa ni afisa huyo akiburuzwa mchangani
na kuteswa na wanaodhaniwa kuwa magenge wa Haiti, msemaji wa MSS aliipuzilia
mbali video hiyo akisema kwamba huenda si ya kweli.
Kwa mujibu wa Ombaka, walipofika Haiti
walikuta kwamba magenge hao walikuwa wanatumia sana propaganda kuzua hofu na
woga kwao, jambo ambalo wamefanikiwa kulizima kwa asilimia kubwa.
Ombaka alitilia shaka video hiyo akisema
kuwa huenda ni ya AI na si ya kweli kwamba ni afisa wao – Benedict Kabiru.
“Kitu kimoja ambacho ni cha wazi
hapa Haiti ni kwamba wengi wa magenge ya Haiti hujiendeleza kwa kutumia propaganda.
Hiyo video inayosambazwa na haswa katika wakati huu wa ujio wa AI, kuna
uwezekano mkubwa kwamba hiyo video ni ya Benedict Kabiru,”
Ombaka alisisitiza.
Idara ya polisi humu nchini, NPS wiki
mbili zilizopita ilitoa taarifa kuhusu kutoweka kwa afisa huyo wa polisi wakati
genge la Haiti lilishambulia msafara wao uliokwama kwenye shimo linalokisiwa
kuchimbwa barabarani makusudi na magenge hayo.
Tangu wakati huo, kumekuwa na uvumi
mitandaoni kwamba huenda afisa huyo aliuawa na mwili wake kufichwa na magenge
hao, lakini NPS na MSS wamesimama imara kukanusha wakisema kwamba juhudi za
kumtafuta zingalipo na atapatikana akiwa hai.