
Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, almaarufu Jicho Pevu, amesema yuko huru kutangamana na kila mtu akiwemo Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Ali alisema hayo siku ya Jumatatu wakati akidokeza kukihama chama cha UDA, akitaja tofauti na baadhi ya viongozi.
Mbunge huyo alidai kulikuwa na mipango ya kumzuia kugombea kwa tiketi ya chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu wa 2027.
Ali alisema alikuwa akishambuliwa na baadhi ya viongozi wa UDA ambao, alisema, wanadai alikuwa na uhusiano wa karibu na Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.
"Katika jumbe za arafa, wananiita mtu wa Wamunyoro, huyo ndiye mimi. Hakuna ubaya kuwa na rafiki. Rigathi Gachagua alikuwa sehemu ya timu yetu. Alipigania UDA. Alikuwa Naibu Rais," alisema.
"Aliondolewa; yuko nje akiendelea na siasa zake. Hakuna mtu ambaye atanizuia kuzungumza naye na kunywa chai naye."
Matamshi yake yanajiri siku chache tu baada ya kutangaza kuwa yeye na timu yake ya kisiasa hawatashiriki uchaguzi wa mashinani, akitaja ukosefu wa ushirikishwaji katika mchakato wa uchaguzi.
Alielezea wasiwasi wake juu ya kutengwa kwa wale waliosaidia chama kukua hadi kufikia hadhi ya sasa.
"UDA, kama chama kingine chochote cha siasa, ni mali ya wananchi, si mtu yeyote, bila kujali wadhifa wake," alisema.
Hii si mara ya kwanza kwa mbunge huyo kudokeza kufanya kazi na Gachagua.
Mnamo Oktoba 2024, mbunge huyo alisema alikuwa mmoja wa wabunge walioshindwa kutia saini hoja ya kumshtaki aliyekuwa DP.